Kumekucha Daraja la Magufuli, Ulega aeleza Rais Samia atakavyozindua

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 05:22 PM May 20 2025
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega.
Picha: Mtandao
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa Daraja la John Magufuli (Kigongo-Busisi) itakaofanyika Juni 19 mwaka huu.

Ulega ameyasema hayo leo katika mkutano wa hadhara wilayani Sengerema mkoani Mwanza wakati akizungumza mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ambaye yuko ziarani mkoani humo.
 
Waziri Ulega amewataka wananchi wa Mwanza kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi huo wa daraja hilo lenye urefu wa kilometa tatu linalotarajiwa kuwa refu kuliko yote katika eneo la Afrika Mashariki na Kati.
 
“Kukamilika kwa daraja hili ni mafanikio ya maono na jitihada kubwa zilizofanywa na Rais Samia na mtangulizi wake, hayati John Magufuli,” amesema.
 
“Namna pekee ya kuonyesha furaha yetu na shukrani zetu kwa mafanikio hayo ni kwenu wananchi wa Sengerema, mkoa wa Mwanza, Geita, mikoa yote ya Kanda ya Ziwa na wa Tanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kwenye uzinduzi huo,” amesema.
 
Ziara ya Waziri Mkuu mkoani Mwanza ni ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambako Ulega alitumia mkutano wa Sengerema kumweleza Waziri Majaliwa kwamba kukamilika kwa daraja hilo kutarahisisha huduma za usafiri na uchukuzi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa ujumla.
 
“Watu waliokuwa wanasafiri kwa zaidi ya saa mbili watakwenda kusafiri kwa wastani wa dakika tatu hadi tano, tunamshukuru rais kwa maono na maelekezo yake,” amesema.
 
Ameongeza kuwa zaidi ya Sh. Bilioni 700 zimetumika katika ujenzi wa daraja hilo linalounganisha mji wa Kigongo na Busisi katika Ziwa Victoria ambalo ni la tatu kwa ukubwa duniani.
 
Aidha, Waziri Ulega amewahakikishia wakazi wa Wilaya ya Sengerema kuhusu ujenzi wa barabara Segerema - Nyehunge kwa kiwango cha lami, akisisitiza kuwa serikali iko katika hatua za mwisho za kumkabidhi mkandarasi kazi ya ujenzi huo.