Mmoja wa majeruhi wa ajali ya mgodi wa Mwakitolyo namba 8, wilayani Shinyanga, Nkwabi Bugisi, amekatwa mguu wa kulia baada ya kuumia vibaya katika ajali hiyo, huku Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, akitoa onyo kali dhidi ya upotoshaji wa taarifa zinazohusu tukio hilo.
Akizungumza leo Mei 20 na waandishi wa habari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Mganga Mfawidhi Dk. Luzila John, amesema kuwa ajali hiyo ilitokea Mei 17, na hospitali ilipokea majeruhi saba mnamo Mei 18 saa 8 usiku.
“Majeruhi wanne walitibiwa na kuruhusiwa baada ya hali zao kuwa nzuri. Mgonjwa mmoja alipewa rufaa kwenda Hospitali ya Bugando, na mmoja, Nkwabi Bugisi, alilazimika kufanyiwa upasuaji wa kukatwa mguu wa kulia kutokana na majeraha makubwa,” amesema Dk. Luzila.
Ameongeza kuwa kwa sasa hospitali hiyo imebakiwa na wagonjwa wawili ambao wanaendelea na matibabu.
Mmoja wa majeruhi, Zacharia Bachangwana, ameeleza kuwa ajali hiyo ilitokea walipokuwa katika shughuli za kutafuta madini kwa kuokota mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu, ndipo gema la mgodi lilianguka na kuwafunika.
“Gema lilipoanguka, kila mmoja wetu alijaribu kujiokoa. Mawe mazito yaliwakandamiza baadhi ya wenzetu, nami nikiwa mmoja wa waliojeruhiwa vibaya,” amesema Bachangwana.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amefafanua kuwa tukio hilo liliwahusisha watu 17, siyo 150 kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.
“Katika tukio hilo, watu 6 walifariki dunia na 11 walijeruhiwa. Haya ni maisha ya watu, si jambo la kufanyia mzaha au kusambaza taarifa za uongo,” ameonya.
Macha amewataja waliopoteza maisha kuwa ni Ntemi Costantine, Agnes Zabroni, Mponeja Sabato, Patrick Kanizio, Haji Juma, na mwanaume mmoja ambaye bado hajafahamika. Miili mitano kati ya hiyo tayari imetambuliwa na kuchukuliwa na ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi.
Ajali hiyo ilitokea Mei 17, baada ya gema la mgodi huo kuanguka wakati wachimbaji wakiendelea na shughuli za utafutaji madini, na kuleta maafa hayo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED