Ujumuishi watumishi wenye mahitaji maalumu wapongezwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:01 PM Apr 29 2025
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, amepongeza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), kuwajali watu wenye mahitaji maalum kwa kuwapa kipaumbele kama walivyo watumishi wengine.

Hayo ameyasema leo Aprili 29, 2025, mkoani Singida alipotembelea banda la WCF katika Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, yanayoendelea mkoani humo.

Kikwete amekutana na kuongea na wafanyakazi wenye mahitaji maalumu ambao ni waajiriwa wa WCF na ameridhishwa na utendaji wao ambao umefanywa na mfuko huo.

Ujumuishi watumishi wenye mahitaji maalumu wapongezwa
Baadhi ya watumishi hao wameeleza namna WCF inavyowajumuisha kikamilifu katika kila hatua na matukio yote yanayohusisha wafanyakazi na kuwawezesha kwa kuwapatia vifaa wezeshi vinavyowarahisishia kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

“Nilipoanza kazi WCF, waliniuliza vifaa ninavyohitaji katika kutekeleza majukumu yangu, niliwaeleza na nilipatiwa vifaa hivyo na kwa sasa ninaendelea kutekeleza majukumu yangu kikamilifu” 

Pia, Kikwete amesema jitihada za kuimarisha usawa na ujumuishaji mahali pa kazi zinaonekana na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu na huduma bora zaidi kwa wafanyakazi wote.

Maadhimisho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, yanayoendelea mkoani Singida
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF Dk. Abdulsalaam Omar, amesema kuwa WCF itaendelea kuwajumuisha wafanyakazi wenye mahitaji maalumu na kuhakikisha mazingira yao ya kazi yanakuwa salama kama ilivyo kwa wafanyakazi wote.