Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Wilaya ya Tunduru (TAMCU), Mussa Manjaule, amewataka wakulima wa zao la korosho kufanya palizi kwa bidii kwenye mashamba yao, wakati huu ambapo viuatilifu na pembejeo za msimu ujao zimeanza kuwasili wilayani humo.
Akizungumza wakati wa kutoa taarifa hiyo, Manjaule amesema kuwa gari la kwanza lililobeba shehena ya viuatilifu hivyo tayari limewasili na kushusha mizigo katika maghala ya Mindu, huku magari mengine yakiendelea kusambaza pembejeo hizo katika maeneo yote ya wilaya kama ilivyopangwa.
"Kwa sasa tunaendelea kuhakikisha kila mkulima anapata pembejeo kwa wakati. Hii ni sehemu ya juhudi zetu kuwahakikishia wakulima upatikanaji wa viuatilifu mapema ili kuongeza uzalishaji," amesema Manjaule.
Amefafanua kuwa tayari TAMCU imeagiza tani 60,000 za viuatilifu kwa ajili ya kupulizia mikorosho ya wakulima katika msimu huu wa kilimo, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha ongezeko la uzalishaji linaendelea kudumu.
Kutokana na hali hiyo, Manjaule amewataka wakulima kuendelea na kazi ya kupalilia mashamba yao na kuepuka kuyaacha kuwa pori. Pia alihamasisha kuongeza ukubwa wa mashamba ili kuongeza uzalishaji na kipato kwa kaya zao.
"Mkulima wa korosho ni sekta muhimu katika taifa letu, hasa katika kuchangia pato la taifa na fedha za kigeni. Tunapaswa kujivunia na kutembea kifua mbele," amesisitiza.
Katika hotuba hiyo, Manjaule aliwapongeza wakulima wa vijijini kupitia vyama vya msingi (AMCOS) na chama kikuu TAMCU kwa juhudi zao katika kuzalisha korosho na mazao mchanganyiko yenye ubora.
Amesema juhudi hizo zimechangia ongezeko kubwa la uzalishaji kutoka tani 180,000 msimu wa 2022/2023 hadi kufikia tani 520,000 msimu wa 2024/2025.
Kutokana na mafanikio hayo, Manjaule amevitaka vyama vya msingi kushirikiana na vyama vikuu katika kutoa elimu kwa wakulima juu ya kuongeza tija, kuachana na mashamba pori, na kuelekea kwenye mnyororo wa thamani kwa kujenga viwanda vya ubanguaji ili kuongeza thamani ya mazao na kipato cha mkulima.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED