Kadinali Giovanni Angelo Becciu, aliyewahi kuwa mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa ndani ya Vatican, ametangaza rasmi kuwa hatashiriki katika mkutano wa siri wa kumchagua Papa mpya, licha ya jitihada zake za awali kurejeshewa haki hiyo.
Kadinali Becciu alikumbwa na kashfa ya kifedha iliyosababisha Papa Francis mwaka 2020 kumuondolea hadhi na haki zote za ukadinali, hatua ambayo ilimzuia kushiriki katika mikutano muhimu ya kanisa, ikiwemo ule wa kumchagua kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki.
Baada ya kifo cha Papa wiki iliyopita, Becciu alikata rufaa akitaka kuruhusiwa kushiriki katika mkutano huo muhimu wa uchaguzi wa Papa, lakini mnamo Aprili 29 alitoa taarifa rasmi akitangaza kujiondoa.
“Nimeamua kutii, kama ambavyo nimekuwa nikifanya daima, mapenzi ya Papa Francis ya kutoniruhusu kushiriki katika mkutano wa siri, huku nikiendelea kushikilia kuwa mimi si mwenye hatia,” alisema Kadinali huyo katika taarifa yake.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Vatican iliyotolewa Jumatatu, makadinali wanatarajiwa kuanza mkutano huo wa siri tarehe 7 Mei, kwa ajili ya kumchagua Papa mpya wa Kanisa Katoliki, ambalo lina waumini takribani bilioni 1.4 duniani kote.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED