WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema serikali imeanzisha mchakato wa kuandaa Sera ya Akili Mnemba, ili kuhakikisha teknolojia hiyo inaendana na misingi ya uhuru wa vyombo vya habari, uwazi na uadilifu.
Majaliwa amebainisha hayo, leo, Aprili 29, 2025, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yanayofanyika jijini Arusha.
Amesema sambamba na mchakato wa kuandaa sera hiyo, serikali pia inaendelea kupitia upya Sera ya Habari na Utangazaji ya Mwaka 2003, ili kuhakikisha inaimarisha na kulinda taaluma ya uandishi wa habari nchini.
Amewasihi pia waandishi wa habari kutumia teknolojia ya akili mnemba kama nyenzo ya kuwasaidia kutekeleza majukumu yao, badala ya kuwa kikwazo kwa uhuru wa habari.
Aidha, amesema serikali itaendelea kulinda uhuru wa habari kwa vitendo, kwa kushirikiana na waandishi wa habari, na kwamba tayari wameunda kamati ya kutathmini hali ya tasnia hiyo na kutatua changamoto zake.
Ametoa pia wito kwa waandishi wa habari, kuzipa kipaumbele taarifa zinazolinda maadili, kukuza uchumi na kuendeleza utamaduni wa taifa.
Katika hatua nyingine, amesema serikali itashirikiana kwa karibu na vyombo vya habari kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa 2025, kupitia Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwamba uchaguzi huo unafanyika kwa uhuru, amani, haki na uwazi.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Paramagamba Kabudi, amewataka waandishi wa habari, kwamba wasitegemee tu teknolojia ya akili mnemba, bali waendelee kutumia uwezo wao wa kiakili katika kuchakata na kuandaa maudhui ya habari.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Greyson Msigwa, amewapongeza waandishi wa habari, kwa kutekeleza majukumu yao, licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali, huku akiwaasa wasikate tamaa kwani wao ni nguzo ya matumaini kwa wananchi.
Awali, Mwenyekiti wa maadhimisho hayo, Maxence Melo, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Africa, akiwasilisha baadhi ya maazimio ya mijadala, amesema wadau walipendelezwa kufanyike mapitio upya ya Sera ya Habari na Utangazaji ya Mwaka 2003, ili iendane na maendeleo ya teknolojia ya akili mnemba.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Mwaka 2025 inasema "Athari za Akili Mnemba kwa Uhuru wa Vyombo vya Habari na Tasnia ya Habari."
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED