Wanachama IPP wamburuza Msajili,Mwanasheria Mkuu mahakamani

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 07:28 PM Apr 29 2025
Wanachama wawili wa Chama cha Siasa cha Independent People's Party (IPP), Vyonheaven Urima na Andrew Bomani.
Picha: Nipashe Digital
Wanachama wawili wa Chama cha Siasa cha Independent People's Party (IPP), Vyonheaven Urima na Andrew Bomani.

Wanachama wawili wa Chama cha Siasa cha Independent People's Party (IPP), Vyonheaven Urima na Andrew Bomani, wamewasilisha maombi Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, wakiomba ruhusa ya kufungua shauri la mapitio dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Urima na Bomani wanadai kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa ameshindwa kukipa usajili wa muda chama chao kwa zaidi ya mwaka mmoja, hali ambayo imezua mashaka kuhusu utekelezaji wa wajibu wa kisheria wa ofisi hiyo.

Kupitia maombi hayo, wanaiomba Mahakama iwape ruhusa ya kufungua shauri la kuomba amri ya Mandamus — amri ya Mahakama inayolazimisha mamlaka ya serikali kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

Vilevile, wanaiomba Mahakama iwape ruhusa hiyo ili kufungua rasmi shauri la mapitio ya uamuzi wa Serikali, wakieleza kuwa uamuzi wa Msajili umekiuka haki zao kama waombaji wa usajili wa chama kipya cha siasa.

Shauri hilo la madai limepewa namba 8386/2025 na linatarajiwa kutajwa mbele ya Jaji Obadia Bwegoge Mei 22, 2025 saa 2:30 asubuhi.

Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali tayari wamepelekewa wito wa kufika mahakamani siku hiyo bila kukosa. Aidha, wameelekezwa kuwasilisha nyaraka zote ambazo wanakusudia kuzitumia kama vielelezo katika shauri hilo.