Wasira: CCM haitasaidia wabunge wazembe

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 10:31 PM Apr 18 2025


Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Stephen Wasira
Picha: Maulid Mmbaga
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Stephen Wasira

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Stephen Wasira, amesema chama hicho hakitakuwa na namna ya kuwasaidia wabunge wazembe, badala yake kitaweka mbele maslahi mapana ya wananchi kwa kuchagua mbunge wanaomkubali.

Akizungumza na wana CCM mkoani Tabora leo Wasira amesema CCM hakitakuwa na namna ya kuwasaidia wabunge wake waliopewa nafasi ya kuwawakilisha wananchi lakini wakashindwa kuitendea haki.

Amesema msimamo wake kwa sasa ni kupata wagombea wanaokubalika na wananchi ndio maana kimebadili utaratibu wa kura za maoni na mchujo.

"Tunataka kazi yetu iwe rahisi, tunataka mgombea ubunge mwenzetu ambaye pia akienda kwa wananchi ni mwenzao kwasababu hawezi kusahau kurudi kwa wenzake. 


“Mtu aliyefanya vizuri huwezi kuwaambia wananchi ulikuwepo. Ulikuwepo sawa, lakini kama maoni hayaendi sawa utatusamehe, maana tunataka yule ambaye alifanya vizuri. Kama hukufanya vizuri sasa tutakusaidiaje," amesema Wasira.


Ameongeza kuwa “CCM tulikupeleka na kuchaguliwa, lakini baada ya kuchaguliwa ukapotea. Umefika wakati wa uchaguzi unasema ‘nimerudi nyumbani’, ulienda wapi? Na kama kweli ulisafiri kwa nini hukuwaaga waajiri wako?”

Amesema kwa sasa wanajua kuwa wako ambao wanapitapita, wanawafahamu na wanawafuatili mwenendo wao. Na kwamba hawafuatilii waliopo tu bali hata wa zamani, maana kuna mambo hayawaridhishi.

“Siku hizi hakuna kupita bila kupingwa, sheria imekataa. Kwa hiyo hata ukifanya kuzuia wengine unapoteza muda, acha waje kama ni 10 au 20," amesema Wasira.