Kanuni za uchaguzi rasmi Gazeti la Serikali

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:10 PM Apr 18 2025
Kanuni za uchaguzi rasmi Gazeti la Serikali
Picha:Mtandao
Kanuni za uchaguzi rasmi Gazeti la Serikali

Kwa sasa ni mguu sawa kwa vyama 18 vilivyosaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani Aprili 12,mwaka huu,baada ya kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali Toleo namba 16 la Aprili 18,2025.

Kanuni hizo kwenye Gazeti la Serikali ni za Tangazo la Serikali Namba 249 la.mwaka 2025, amabzo zina vipengele saba vyenye vipengele vidogo vidogo.

Kamuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025 ambazo katika ukurasa wa kwanza zimeweka msingi unaopaswa kuzingatiwa na washiriki wa uchaguzi pamoja na hatua za kinidhamu zinazoweza kuchukuliwa kwa atakayekiuka Kanuni hizi.

Kanuni hizi za Maadili zitatumika katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, kuanzia siku moja baada ya tarehe ya uteuzi wa wagombea wa uchaguzi mkuu hadi baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo.

Vilevile, Kanuni hizi zitatumika katika chaguzi ndogo zitakazofuata na kwamba wahusika ni wagombea Rais, Wabunge na Madiwani.

Aidha,kanuni hizo zinaeleza kuhusu wajibu kusaini na kuthibitisha kuheshimu kanuni za maadili.

Kwamba kila chama cha siasa, serikali na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi watawajibika kusaini Kanuni hizi za Maadili.

"Chama cha siasa ambacho hakitasaini Kanuni hizi za Maadili kitazuiliwa kushiriki katika uchaguzi,"sehemu ya kanuni hizo.

Aidha, kila mgombea, kabla ya kuteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi atathibitisha kuheshimu na kutekeleza Kanuni hizi za Maadili kwa kujaza.

Vile vile watatakiwa kusaini Fomu Na.10. iliyoainishwa katika jedwali la kwanza la kanuni mbele ya Mkurugenzi wa Uchaguzi, msimamizi wa uchaguzi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi kadiri itakavyokuwa. Fomu hiyo itatolewa na Tume au msimamizi wa uchaguzi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi na itarejeshwa pamoja na fomu ya uteuzi.