Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakina mgogoro na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kumwomba Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba kuwa msuluhishi wa yanayoendelea ndani ya chama hicho cha upinzani.
Amesema Mzee Warioba anao uwezo wa kumaliza mgogoro ndani ya CHADEMA na kwamba, CCM ikisikia kama kuna mchango unahitajika watasaidia ili chama hicho warudi kuwa wamoja kwa sababu kwa sasa inasikitisha.
Mwishoni mwa wiki, Jaji Warioba alishauri serikali na CHADEMA kukaa meza ya moja ha mazungumzo ili kupata muafaka wa amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Akizungumza leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mikese, mkoani humo ikiwa ni siku yake ya kwanza ya ziara yake ya siku saba, Makalla amesema CCM inaheshimu ushauri wa Jaji Warioba aliotoa mwishoni mwa wiki, na kueleza kuwa CCM ina uhusiano mzuri na CHADEMA.
Makalla amesema juzi amemsikiliza Jaji Warioba ambaye wanamheshimu amekuwa Waziri Mkuu na mbobezi wa mambo ya uongozi na mwanasheria nguli na mwenye mchango katika taifa.
“Anaheshimika ni miongoni mwa wazee ambao tuko nao na wakati wote tutaendelea kuheshimu michango yao, nimemsikia akieleza, akitoa ushauri kwamba CCM wakae CHADEMA wamalize mgogoro kisiasa.
“Kama nilivyosema tunamheshimu, ametoa ushauri mzuri wa sisi kukaa na CHADEMA kuongelea mgogoro wa kisiasa.
“Ninataka nimwaambie ushauri wake tumeupokea, lakini hauwezi ukatumika sasa kwa sababu CCM hatuna mgogoro wa kisiasa na CHADEMA,” amesema.
Makalla amesema ushauri wake unaweza kuja kutumika huko ikitokea CCM ina mgogoro kisiasa na CHADEMA.
Amesema Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) inayohusisha vyama vyote vya kisiasa ambako huongelea mambo yote ya siasa, Mwenyekiti wake ni wa CHADEMA, hivyo mambo yao wanaongea vizuri na huipa nafasi CCM kutoa maoni yake.
“Ushauri aliotoa Mzee Warioba mimi ninamwomba kwa kuwa CCM haina mgogoro na CHADEMA naomba ushauri aliotoa akawe msuluhishi akaisuluishe CHADEMA ambayo tangu uchaguzi ina makundi, kinasambarati.
“Ni muda wa Mzee Warioba sasa tumpeke pale akae nao na G55 na kina (Freeman) Mbowe, Tundi Lissu awasuluhishe na CCM kipo tayari kuchangia mchango wa kumaliza mgogoro ndani ya CHADEMA,” amesema.
Makalla amesema anaamini kwa busara alizonazo Mzee Warioba anaouwezo wa kumaliza mgogoro ndani ya CHADEMA,na kwamba CCM ikisikia kama kuna mchango unahitajika watasaidia ili chama Hicho warudi kuwa wamoja kwa sababu kwa sasa inasikitisha.
Amesisitiza kuwa mzee Warioba hiyo kazi anaiweza na kueleza kuwa CCM haina mgogoro na chama hicho kikuu cha upinzani.
Jaji Warioba alitoa ushauri huo mwishoni mwa wiki katika Kongamano la Kitaifa la Uchaguzi Mkuu lililoandaliwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED