Makalla: Kuna watu wanajizima data mradi SGR

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 01:55 PM May 05 2025
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla.
Picha: Mtandao
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla, amesema ameamua kutumia usafiri wa SGR kusafiri kudhibitisha kazi nzuri zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa wakati mwingine kuna watu wanajizima data.

Ameyasema hayo leo mkoani humo, ikiwa ni siku yake ya kwanza ya ziara ya siku saba katika mkoa huo, ambapo baadaye jioni atafanya mkutano wa hadhara utakaofanyika Mikese.

“Hawaoni kama kuna SGR wakipanda wanajificha nyuso zao. Walipinga wakati wa kujenga SGR, lakini chini ya usimamizi wa Rais Samia amekamilisha kipande hiki Dar es Salaam-Morogoro na Morogoro-Dodoma kwa sasa usafiri ni safi,” amesema.

Makalla amesema Rais Samia aliahidi wakati anaongea bungeni kwamba, ataendeleza miradi yote ya awamu ya tano iliyoasisiwa na Hayati Rais John Magufuli.

“Rais Samia ametekeleza na amedhibitisha na kukamilisha SGR kipande cha Dar es Salaam- Morogoro na amekamilisha pia, Morogoro-Dodoma  na ameanzisha vipande vingine mpaka Mwanza, Tabora hadi Kigoma,”

Makalla amesema anayesema haoni maendeleo anatakiwa kupimwa akili kwa kuwa wao wanaona na wanaendelea kuwakumbusha wananchi kwamba,  mafanikio hayo yote ni mipango mizuri ya utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Amesema wengine hawana wajibu wala dhamana zaidi ya CCM ambacho kinatekeleza kwa vitendo kuwaletea wananchi maendeleo.

1