Aliyeposti ‘siku za Kitima zinahesabika’ mbaroni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:37 PM May 05 2025
 Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Saalam,Jumanne Muliro
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Saalam,Jumanne Muliro

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaama, limemkamatwa pia na kumhoji kwa kina Mkazi wa Dodoma na Mbezi Makonde Dar es Salaam, Frey Edward Cossey (51) kufuatia chapisho lake la vitisho dhidi ya Padri Charles Kitima alilolitoa kwenye mitandao ya kijamii siku chache kabla ya tukio.

Taarifa kwa umma iliyotolewa leo Mei 5,2025 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Saalam,Jumanne Muliro,imeeleza kuwa upelelezi wa shauri la Padri Kitima unaendelea.

"Jeshi la Polisi linawashukuru wananchi na linatoa wito kuendelea kushirikiana, ili kuimarisha mifumo ya usalama na kutotoa fursa kwa wahalifu kutenda makosa,"amesema.


Padri Kitima alishambuliwa na kitu kizito Aprili 30,2025 usiku katika Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Kurasini,na anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Agakhan Dar es Salaam.

Tangu kutokea kwa tukio hilo kumekuwa na kauli za ndani na nje za kulaani shambulio hilo baya dhidi ya kiongozi wa dini,huku kila mmoja akitaka hatua madhubuti zichukuliwe ikiwamo kuwakamata waliohusika.

Aidha, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa aliagiza aliyeandika 'Siku za Kitima zinahesabika' akamatwe.

Taarifa ya Mei mosi,2025 ya Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ilieleza kuwa watu wawili wamehusika na tukio hilo na mmona anashikiliwa.