Katika maadhimisho ya miaka 11 tangu kuzaliwa kwa ACT Wazalendo, Kiongozi wa Chama hicho, Dorothy Semu, amesema chama hicho kimejenga jukwaa mbadala na la kuaminika kwa Watanzania wote, na kuwa ndio chombo kinachoaminika kuleta ukombozi wa kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Akihutubia kwenye Ukumbi wa Hakainde Hichilema, Makao Makuu ya Chama jijini Dar es Salaam, Dorothy amesema kuwa licha ya changamoto nyingi, ACT Wazalendo imepiga hatua kubwa katika miaka 11, na sasa ni chama kinachokua kwa kasi zaidi nchini.
Akitaja mafanikio 10 makubwa ya chama hicho, Dorothy ameeleza kuwa ACT Wazalendo imeongoza siasa za hoja, kujenga jukwaa kwa wanasiasa wa siasa safi, kuwaamini vijana, kuendeleza ukombozi wa wanawake, kuwa sauti ya matumaini kwa makundi mbalimbali na kuwa chombo cha kupigania haki za binadamu.
Aidha, amesisitiza kuwa mwaka 2025 ni wa kipekee kwa sababu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, na chama hicho kimejiandaa kushiriki kikamilifu. Amesema uamuzi wa kushiriki ni wa kimkakati ili kulinda thamani ya kura, kukataa udikteta na kuwa tayari kuiongoza nchi baada ya kushindwa kwa CCM kwa zaidi ya miongo sita.
Dorothy ametangaza majukumu matatu makuu ya ACT Wazalendo kuelekea uchaguzi: kupigania malengo ya chama, kupigania maboresho ya mfumo wa uchaguzi, na kuunganisha taifa. Amewataka wanachama wasitetereke bali wasimame imara, hususan kwa upande wa Zanzibar, ambako amesema wananchi wamechoka na utawala wa Rais Mwinyi.
Amesisitiza kuwa chama hicho kitapaza sauti hadi uchaguzi uwe huru na wa haki, huku akiorodhesha madai sita ya msingi: kuondolewa kwa wakurugenzi kama wasimamizi wa uchaguzi, uteuzi mpya wa Tume ya Uchaguzi, kudhibiti kura haramu, kuepuka kuengua wagombea kiholela, kuhakikisha uhuru wa mawakala na kuzuia vyombo vya dola kuingilia uchaguzi.
Katika kuhitimisha, Dorothy ametoa wito kwa Rais Samia kuisikiliza sauti ya viongozi wa dini na wito wa haki, akisema kwamba hilo ndilo suluhisho la kulinusuru taifa kuelekea 2025. Amesema ACT Wazalendo itaendelea kujenga jukwaa la ukombozi, kwa Tanzania na Zanzibar yenye mamlaka kamili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED