Serikali imepiga marufuku matumizi ya mashine aina ya msumeno mnyororo (chain saw) kutumika kukatia miti bila kibali kutoka mamlaka husika ili kupunguza kasi ya uharibifu wa uoto wa asili na mazingira kwa ujumla.
Pia, imesema ili kukabiliana na janga la ukataji holela wa miti, hekta takribani millioni 5.2 za maeneo yaliyoharibiwa zinatarajiwa kupandwa miti ifikapo mwaka 2030.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Patrobas Katambi amesema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Swali hilo lililoulizwa na Mbunge wa Moshi Vijijini Prof. Patrick Alois Ndakidemi aliyetaka kujua tamko la serikali kwa watu wanaovuna miti kwa kutumia misumeno mnyororo na hivyo kuwa kikwazo katika juhudi za kuhifadhi mazingira.
Akijibu swali hilo, Katambi amesema kuwa pamoja na kwamba mashine hizo zinauzwa nchini upo utaratibu maalumu unaotoa mwongozo wa kufuata zisitumike ovyo kwenye maeneo ambayo hayajatolewa vibali.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais nitoe maelekezo ni marufuku kwa mtu yeyote kutumia chain saw bila kibali kutoka mamlaka zilizopo kwenye maeneo husika inayotambulika kisheria, kuna utaratibu wa namna ya kufanya uvunaji, tunaomba wazingatie hili kwani kwa ukiukaji wa taratibu hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” amesisitiza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED