Rais wa Marekani Donald Trump amekanusha kuwa anafikiria muhula wa tatu wa urais, hatua ambayo wataalamu wanakubali kuwa ni marufuku kwa mujibu wa Katiba ya Marekani.
“Nitakuwa rais kwa miaka minane, nitakuwa rais wa awamu mbili. Siku zote nilifikiri hilo lilikuwa jambo muhimu sana,” Trump alisema katika mahojiano na kipindi cha Meet the Press cha NBC, yaliyofanywa na Kristen Welker na kurushwa hewani Jumapili.
Trump, mwenye umri wa miaka 78, hapo awali alishawahi kusema kwamba "hakuwa anatania" kuhusu wazo la kuhudumu muhula wa tatu, au hata wa nne kama Rais wa Marekani.
Hata hivyo, baadaye alifafanua kuwa kauli hizo zililenga kuudhi "vyombo vya habari bandia".
Licha ya kauli zake za kukanusha, kampuni yake — The Trump Organization — imekuwa ikiuza kofia zenye maandishi ya "Trump 2028", hatua ambayo imezua maswali na uvumi kuhusu uwezekano wa kutaka kuendelea na madaraka hata baada ya kumaliza muhula wa pili unaotarajiwa kukamilika Januari 2029.
Katika mahojiano hayo yaliyorekodiwa Ijumaa kutoka nyumbani kwake huko Florida, Trump alidai kupokea “maombi mengi” kutoka kwa watu wanaomtaka afikirie kusalia ofisini zaidi ya mihula miwili.
“Watu wengi wanataka nifanye hivyo,” alisema Trump, siku chache tu baada ya kusherehekea siku 100 za kwanza za muhula wake wa pili.
“Ni kitu ambacho, kwa uelewa wangu, hakiruhusiwi kufanyika. Sijui kama hiyo ni marufuku ya kikatiba au kuna sababu nyingine yoyote,” aliongeza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED