Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amesema baada ya ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi kukamilika kwa asilimia 99 utaenda kufanikisha kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi Kanda ya Ziwa na nchi jirani.
Waziri Ulega ameyasema hayo leo Bungeni Dodoma, wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka 2025-26, akieleza kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutakuwa faraja kubwa kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa ambao wamekuwa wakitumia muda wa takribani saa mbili kuvuka kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine.
"Baada ya daraja hili kukamilila muda wa kuvuka unatarajiwa kupungua kufikia wastani wa dakika tatu. Aidha daraja hili linategemewa kuongeza shughuli za kiuchumi ndani na nje ya mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani.Pia daraja hili litakuwa mojawapo ya alama na fahari ya taifa letu kwani kwa urefu wake wa Kilomita 3.2 litakuwa daraja refu zaidi katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki na kati," amesema Waziri Ulega.
Waziri Ulega ameeleza kuwa baada ya kuzinduliwa kwa daraja hilo na kuanza kutumika kikamilifu, vivuko vyote vilivyokuwa vinatumika kwenye eneo hilo la Kigongo-Busisi vitapelekwa katika maeneo mengine nchini yatakayokuwa na uhitaji wa huduma hiyo.
Kadhalika amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan ambaye si tu amelupa gharama zote kwa wakati kwa mkandarasi wa mradi huo lakini pia amekamilisha mradi huo ambao ulikuwa ni ndoto ya mtangulizi wake Hayati John Pombe Magufuli.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED