ACT Wazalendo yajivunia mambo 10 ikiadhimisha miaka 11

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:53 PM May 05 2025
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu
Picha: Mpigapicha Wetu
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, amewaongoza wanachama na viongozi wa Chama hicho katika maadhimisho ya miaka 11 ya ACT Wazalendo tangu kipate usajili wa kudumu mnamo Mei 5, 2014.

Katika hotuba yake wakati wa sherehe ya maadhimisho hayo amesema, licha ya changamoto nyingi, Chama kimejenga msingi imara wa mafanikio makubwa kwa kipindi chote cha miaka 11. Kwa sasa, wachambuzi wengi wanakubaliana kuwa ACT Wazalendo ndicho chama kinachokua kwa kasi zaidi nchini.

Amewapongeza wanachama kwa kazi kubwa ya kukijenga chama hadi kufikia kuwa chombo kinachotumainiwa na Watanzania kuleta mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kisiasa—Tanzania Bara na Zanzibar.

Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa maadhimisho ya miaka 11 ni fursa ya kusherehekea mafanikio makubwa 10 ambayo ACT Wazalendo imeyapata, na ambayo yanaonesha kuwa chama hicho kimepiga hatua kubwa kuliko vyama vingine vyote nchini.

Mafanikio hayo ni;

1️⃣ Siasa za hoja, si vioja!

 Tumeongoza katika siasa za hoja dhidi ya siasa za vioja, vituko na "uchawa" ambazo ndizo zimetawala katika Chama cha Mapinduzi. Daima, ACT Wazalendo tumetanguliza mbele kuzisemea changamoto za Watanzania na kupendekeza majawabu yake kupitia sera zetu makini.

2️⃣ Jukwaa mbadala kwa wanaotafuta siasa safi.

 Tumejenga jukwaa mbadala ambalo ni kimbilio kwa wanasiasa wanaopenda siasa safi na ambao hawaridhishwi na ukandamizwaji wa demokrasia kwenye vyama vyao. Kielelezo cha mafanikio haya ni kumpokea Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad na wenzake mwaka 2019. Kuaminika na jabali la siasa za Afrika Mashariki, Afrika na Dunia Maalim Seif Sharif Hamad (Mungu amlaze mahala pema) ni ishara ya ukomavu wa siasa za ACT Wazalendo.

3️⃣ Nguvu ya vijana.

 Tumejenga jukwaa la kuaminika na vijana. Mara zote, kupitia chaguzi na teuzi zetu, tumetuma salamu kwa vijana wa Tanzania kuwa hiki ni Chama kinachowaamini na kuwapa nafasi vijana kuonesha vipaji vyao vya kiuongozi. Kuchaguliwa kwa Katibu Mkuu mwaka 2020 akiwa na miaka 34 ilikuwa ni alama ya wazi kwa vijana wote kuwa ACT Wazalendo ni jukwaa lao.


4️⃣ Mapinduzi ya usawa wa kijinsia.

 Tumejenga jukwaa la ukombozi wa wanawake. Tumevunja minyororo ya kukandamiza demokrasia kwa kuongoza kwa vitendo dhana ya usawa wa kijinsia kwa kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kijinsia kwenye vyombo vyote vya maamuzi. ACT Wazalendo ndio chama pekee kilichoweka sharti la wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu wa kuchaguliwa kuwa 50/50! Haya ni mapinduzi makubwa kwenye tasnia ya siasa. Kusimama kwangu mbele yenu kama kiongozi namba moja wa Chama ni ishara nyingine kuwa Chama hiki kinawaamini wanawake!

5️⃣ Ukombozi wa Zanzibar.

 Tumejenga jukwaa la kuaminika la ukombozi wa Wazanzibari ili kujenga Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja na yenye mamlaka kamili. ACT Wazalendo inaenda kuwaongoza Wazanzibari kuikomboa nchi yao kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Kwa hakika, 2025 kwetu ni mwaka wa maamuzi!


6️⃣ Maslahi ya wote, Taifa la wote.

 Tumefanikiwa kujenga jukwaa la kupigania Taifa la wote kwa Maslahi ya wote hasa katika kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kuwakomboa wananchi kiuchumi na kijamii. Tumesimama na makundi yote kwenye jamii; wakulima, wafanyakazi, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara, vijana, wanawake, wazee n.k Hawa wote wanaitazama ACT Wazalendo kama sauti ya matumaini.

7️⃣ Watetezi wa haki za binadamu.

 Tumejenga chombo madhubuti cha kupigania haki za binadamu ndani na nje ya mipaka ya nchi.

8️⃣ Demokrasia ya kweli ndani ya Chama.

 Tumeonesha kwa vitendo demokrasia ya ndani ya Chama. Uamuzi wa Chama kuzingatia ukomo wa madaraka wa miaka 10 kwenye Uchaguzi wa ndani ya Chama wa Mwaka 2024 ni mfano wa wazi uliowashinda wengi.

9️⃣ Uwazi na uwajibikaji.

  Tumejenga Chama kinachoongozwa kwa uwazi na uwajibikaji.

🔟 Chama kinachokua kwa kasi zaidi nchini.

 Tumejenga Chama kinachokua kwa kasi zaidi nchini kwa vipimo vya kupokea wanachama, kutanuka kimtandao na ushawishi wake kisiasa ndani na nje ya mipaka ya nchi.

🟢 #Miaka11ACTWazalendo #SiasaSafi #NguvuYaMabadiliko #TeamACT #Zanzibar2025 #Tanzania