MUHAS kuandaa Kambi Maalum ya Afya ya Moyo Mei 21–22, 2025, Mloganzila

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 04:50 PM May 19 2025
Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhabwa.
Picha: Frank Monyo
Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhabwa.

Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimetangaza kuandaa Kambi Maalum ya Afya ya Moyo itakayofanyika kuanzia Mei 21 hadi Mei 22, 2025 katika Kampasi ya Mloganzila. Wananchi watapata fursa ya kufanyiwa uchunguzi wa awali wa viashiria vya magonjwa ya moyo, uchunguzi wa visababishi, elimu, ushauri wa kitaalamu, pamoja na huduma saidizi kwa wagonjwa wa moyo.

Huduma hizo zitatolewa kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni, na zinalenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kulinda afya ya moyo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 19, Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhabwa, amesema kambi hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu Afrika Mashariki, unaotarajiwa kuzinduliwa rasmi Mei 23, 2025.

“Kambi hii ina kauli mbiu ya ‘Linda Afya ya Moyo Wako’ na inakuja baada ya mafanikio ya awamu ya kwanza, ambayo yalihusisha ujenzi wa jengo la kisasa la kufundishia (Multipurpose Building) pamoja na mafunzo kwa wataalamu wa afya,” amesema Prof. Kamuhabwa.

Ameongeza kuwa awamu ya pili ya mradi inalenga ujenzi wa hospitali ya kisasa ya moyo, uboreshaji wa mitaala ya kitaaluma, tafiti za kina kuhusu kinga, tiba na ukarabati wa magonjwa ya moyo, pamoja na utekelezaji wa programu za kuwafikia wananchi moja kwa moja katika jamii (Community Outreach Programs).

Prof. Kamuhabwa amebainisha kuwa mradi huo ni sehemu ya mpango wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa kuanzisha vituo vya umahiri katika fani mbalimbali, ambapo Tanzania kupitia MUHAS imepewa dhamana ya kuongoza sekta ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.

Mgeni rasmi katika uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Mradi huo anatarajiwa kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.