Lissu avuta hisia za wengi mahakamani, awatuliza wanachama, msilie

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 11:12 AM May 19 2025

Lissu avuta hisia za wengi mahakamani, awatuliza wanachama, msilie
Picha: Iman Nathaniel
Lissu avuta hisia za wengi mahakamani, awatuliza wanachama, msilie

Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu amewasili katika Mahakama ya Kisutu saa 9:41 asubuhi akiwa chini ya ulinzi mkali wa zaidi ya askari Magereza sita.

 Ujio wake uliibua shamrashamra mahakamani, ambapo eneo hilo la kimahakama liligeuka kama uwanja wa hadhara kutokana na msisimko wa waliofika kumsikiliza.

Mara baada ya kufikishwa kizimbani, Lissu alipaza sauti kwa kutumia kauli mbiu maarufu ya CHADEMA, hali iliyopokelewa kwa shangwe na vigelegele kutoka kwa wafuasi wake na wageni waliokuwepo mahakamani. Askari waliokuwa wakimlinda walionekana kushindwa kumzuia wala kuwazuia waliokuwepo ndani ya ukumbi huo wa mahakama.

Lissu alianza kwa kutoa salamu kwa mabalozi waliokuwepo akisema: “Mko vizuri waheshimiwa mabalozi, nawashukuru sana,” kauli iliyopokelewa kwa msisimko mkubwa. Bila kujali uwepo wa ulinzi, aliendelea kuzungumza kwa uhuru kama kwamba yupo katika mkutano wa hadhara.

Aliendelea kwa kusema: “Wanayataka, wameyapata,” huku akionesha nyaraka alizokuwa amezishikilia mkononi na kuongeza, “Mzigo ndio huu hapa.”

Akiendelea na hotuba yake isiyo rasmi, Lissu alisema:
 “Eti wanasema mimi niliwasema vibaya majaji. Waliwahi kumsikia Jaji Warioba aliwasemaje majaji? Eti mimi niliwasema kushinda Warioba?”

Aliwakaribisha waliokuwepo mahakamani kwa maneno ya furaha: “Nafurahi kuwaona wote. Msiogope, kila kitu kitakwenda sawa.”

Kisha akasema: “Jenerali Ulimwengu, I’m happy to see you. Rais Mwambukusi, I’m happy to see you,” huku akiwa bado amezungukwa na askari wa Magereza.

Lissu pia alizungumzia taarifa kwamba Jaji Mkuu wa Kenya amerudishwa uwanja wa ndege ili asije kusikiliza kesi hiyo, akisema: “Sasa mmekwisha.”

Akimtazama mmoja wa viongozi wa chama aliyekuwa na machozi, Lissu alimfariji kwa kusema: “Mwenyekiti unalia? Usilie, huu sio wakati wa kulia.”

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wake kwa kazi kubwa waliyoifanya: “Mmefanya kazi njema sana, hongereni.”

Baadhi ya wanachama wa CHADEMA waliendelea kumpa moyo kwa kupaza sauti: “I love you,” naye Lissu akajibu kwa uchangamfu: “I love you too.”