Sasa barabara lami, madaraja kujengwa jiji la Dar

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 04:57 PM May 19 2025
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo akitoa maelekezo katika moja ya madaraja wilayani humo
Picha: Pilily Kigome
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo akitoa maelekezo katika moja ya madaraja wilayani humo

RAIS Samia Suluhu Hassan, ameidhinisha zaidi ya Sh. bilioni 10 ambazo ni fedha za ndani, kwa ajili ya kujenga miundombinu ya barabara na madaraja wilayani Ilala.

Hayo yamesemwa Mei 18, 2025 jijini Dar es Salaam, na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, mbele ya vyombo vya habari.

Mpogolo amebainisha kuwa wananchi wa wilaya hiyo wanaendelea kunufaika na fedha za ndani ambazo zitaelekezwa katika miradi ya kujengwa kwa madaraja na barabara kwa kiwango cha lami. 

Amezitaja barabara zinazokwenda kunufaika na fedha hizo ni pamoja na barabara ya Tabata Magengeni, daraja la Kavesu na daraja la Mzava zilizopo Kata ya Liwiti.

Barabara ya Faru Mnyamani, Kidarajani, Tatanic moja na mbili zilizopo Kata ya Vingunguti na barabara ya Kigogo Sokoni na Pugu Kanisani zilizopo Kata ya Pugu.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo akitoa maelekezo katika moja ya madaraja wilayani humo
Katika Kata ya Kivule, zinakwenda kujenga daraja la Msumi, Bombambili na Kata ya Kitunda ujenzi wa miundombinu unafanyika katika barabara ya Mwanagati hadi Kitunda. 

Mpogolo ameongeza kuwa kwa upande wa Jimbo la Ilala, Kata ya Kariakoo fedha hizo zimeelekezwa katika ujenzi wa barabara ya Nyamwezi na Congo kwa kiwango cha lami. 

Kata ya Ilala zinakwenda kujenga barabara ya mtaa wa Moshi kwa kiwango cha lami huku Kata ya Buyuni na Chanika, wananchi wananufaika na kujengewa barabara ya Talian Miti Mirefu na Masai Wawili kwa kiwango cha lami. 

Kata nyingine zitakazonufaika ni Kipawa na Buguruni, ambazo ujenzi wa barabara katika kiwango cha lami unafanyika eneo la Airport hadi Karakata na barabara ya Sukita. 

Aidha ametoa wito kwa wakazi wa jimbo hilo, kwa kuwaasa wawe na matumizi mazuri kulinda miundombinu na kuiacha kuifuja.

Pia alitoa wito kwa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) wilayani Ilala, kuhakikisha wakandarasi wote waliopewa tenda za ujenzi wanakabidhi miradi kwa wakati na wahakikishe inaendana na thamani ya fedha zilizotolewa. 

Ameongeza kuwa kupatikana kwa fedha hizo za ndani ni matunda ya serikali na usimamizi mzuri wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kwa ushirikiano wa wabunge na madiwani wote kuhakikisha maendeleo yanaonekana kwa wananchi.