Askofu Lazaro wa TAG afariki dunia

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 10:11 AM May 19 2025

Aliyekuwa Askofu Mkuu wa kwanza mzawa wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God – TAG, Dk. Emmanuel Lazaro.
Picha: Mtandao
Aliyekuwa Askofu Mkuu wa kwanza mzawa wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God – TAG, Dk. Emmanuel Lazaro.

Aliyekuwa Askofu Mkuu wa kwanza mzawa wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God – TAG, Dk. Emmanuel Lazaro, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88.

Askofu Lazaro, alifariki dunia siku ya Jumamosi, tarehe 17 Mei 2025, katika Hospitali ya Rufani ya Kanda ya KCMC iliyoko Moshi, mkoani Kilimanjaro, wakati akipatiwa matibabu.

Marehemu alikuwa kiongozi mashuhuri wa kiroho nchini, aliyesimikwa kuwa mchungaji mwaka 1964, na baadaye kuongoza Kanisa la TAG kama Askofu Mkuu kwa kipindi cha miaka 24, kuanzia mwaka 1967 hadi 1992. Alikuwa kiongozi wa kwanza wa Kanisa hilo kutoka Tanzania, kuchukua nafasi hiyo kutoka kwa wamishenari wa kizungu – hatua iliyoweka historia mpya katika uongozi wa makanisa ya Kipentekoste nchini.

Mbali na nafasi yake ndani ya TAG, Askofu Lazaro, pia alikuwa mwanzilishi wa Kanisa la Kilimanjaro Revival Temple, maarufu kama KRT, ambalo alilianzisha mwaka 1971, na kulitumikia kama Mchungaji Kiongozi hadi alipostaafu.

Askofu Dk. Emmanuel Lazaro atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika kueneza injili, kujenga makanisa, na kulea viongozi wa kiroho ndani na nje ya nchi.