Rais Samia ateuwa makatibu, wenyeviti wa bodi

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 05:00 PM May 19 2025

Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha: Mtandao
Rais Samia Suluhu Hassan.

Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali akiwemo Prof. Tumaini Nagu ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia masuala ya afya.

Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Sharifa Nyanga, Dk. Blandina Kilama ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango anayeshughulikia biashara na ubunifu.

Amesema Dk. Kilama anachukua nafasi ya Dk. Lorah Madete ambaye uteuzi wake umetenguliwa na atapangiwa majukumu mengine.

“Balozi George Madafa ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Puma Energy Tanzania. Akichukua nafasi ya Dk. Majige Budeba ambaye amemaliza muda wake.

“Pia Jacob Kibona ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) kwa kipindi cha pili. Huku Meja Jenerali Mstaafu John Mbungo akiteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) kwa kipindi cha pili,” amesema.

Ameongheza kuwa Mussa Mandia ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kipindi cha pili. Na kwamba uapisho wa Naibu Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mtendaji utafanyika kwa tarehe itakayopangwa.