UWT yahimiza wanawake kuwania uongozi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:14 PM May 19 2025
UWT yahimiza wanawake kuwania uongozi
Picha: Mpigapicha Wetu
UWT yahimiza wanawake kuwania uongozi

KATIBU mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani wa Mara, Zeydani Mwamba, ametoa wito kwa wanawake mkoani humo, kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Amesema  wajitokeze kuwania udiwani, ubunge na nafasi ya viti maalumu katika kipindi cha uchaguzi mkuu utakaofanyika mapema mwezi Oktoba, mwaka huu 2025.

Zeydani ameyabainisha hayo Mei 18, mwaka huu, katika ziara yake katika ukumbi wa CCM uliopo manispaa ya Musoma, mkoani humo, wakati akizungumza na wanawake wanachama wa chama hicho.

"Mfano mzuri ni uchaguzi mdogo uliopita zilitokea kata mbili za kujaza kata ya Mmshikamano na kata ya Mwisenge tuliwahamasisha akina mama tukawaondoa uwoga,tukawaambia washiriki bahati nzuri walishiriki na tukapata kata moja ya Mwisenge aligombea mwanamke na akashinda tayari ni diwani wa kata hiyo" alisema Zeydani.

UWT yahimiza wanawake kuwania uongozi
Zeydani anasema zoezi hilo linaendelea kufanyika akisaidiana na sekretarieti ya UWT mkoani hapa lengo ni kuondoa mfumo dume uliokuwepo mwanzo miongoni mwa wananchi sambamba na hilo aliweka wazi mabadiliko ya kanuni ya ccm kubadilisha mfumo wa wajumbe wanaoshiriki vikao vya maamuzi.

Kw Upande wake Katibu wa UWT wilayani hapa, Teddy Mageni, amesema kuelekea uchaguzi mkuu chama hicho kimepokea maelekezo juu ya zoezi zima la uchaguzi huo na kwamba UWT mkoani humo, imedhamiria kutoa kura za heshima na za mfano kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

"Mama Rais Samia Suluhu Hassan ni mwanamke, UWT Musoma mjini tunaenda na mama Samia tutampa kura za heshima, mwaka huu 2025 tunataka tutoe kura za mfano kwa Mwanamke mwenzetu" anasema  Teddy.

Aidha amewahimiza wanawake na akinamama mkoani humo, kujitokeza kwa wingi na kuchukua fomu ya kushiriki uchaguzi huo, ifikapo Juni, mwaka huu 2025 na kugombea nafasi ya udiwani, ubunge na viti maalumu kuanzia ngazi ya kata na wilaya kwa ujumla