Millen Magese kuandaa Miss Universe Tanzania 2025, BASATA yambariki

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 06:38 PM May 19 2025
Millen Magese kuandaa Miss Universe Tanzania 2025, BASATA yambariki
Picha: Mpigapicha Wetu
Millen Magese kuandaa Miss Universe Tanzania 2025, BASATA yambariki

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limetoa baraka na kibali rasmi kwa Mwanamitindo wa Kimataifa na Mrembo wa zamani wa Tanzania, Millen Happiness Magese, kupitia kampuni yake, kuandaa mashindano ya Miss Universe Tanzania 2025 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa BASATA, Kedmon Mapana, amesema Baraza hilo kama mlezi na msimamizi wa tasnia ya urembo na utanashati nchini, limeridhika na maandalizi ya Magese na kumpatia baraka zote kwa kazi hiyo.

"Tunajivunia kuona mtu kama Millen ambaye anaishi nje ya nchi, lakini bado moyo wake uko nyumbani. Amekuja kurudisha kwa jamii kupitia sanaa ya urembo, jambo ambalo linaongeza thamani ya tasnia yetu," amesema Mapana.

Aidha, Mapana alisisitiza kuwa pamoja na baraka na kibali hicho, BASATA imemkabidhi Millen muongozo wa maadili katika kazi za sanaa, ili kuhakikisha mashindano hayo yanaendeshwa kwa kuzingatia mila, desturi na maadili ya Kitanzania.

"Mashindano ya Miss Universe yana mvuto mkubwa duniani, hivyo ni muhimu mrembo atakayewakilisha nchi awe na maadili yanayoakisi utambulisho wetu kama Watanzania," ameongeza.
1

Millen Magese Atoa Shukrani

Kwa upande wake, Millen Magese ameishukuru BASATA kwa kumuamini na kumpa kibali cha kuandaa mashindano hayo, akieleza kuwa sasa ana baraka zote kutoka BASATA na Miss Universe Organization.

"Hii ni nafasi muhimu kwa Tanzania, kupitia jukwaa hili tutaitangaza nchi yetu kwa watu zaidi ya bilioni moja wanaofuatilia mashindano haya katika mataifa zaidi ya 174," amesema Millen.

Ameongeza kuwa mashindano ya urembo bado ni jukwaa lenye nguvu kubwa ya kimataifa, akiahidi kutumia uzoefu wake wa kimataifa kuboresha zaidi tasnia hiyo nchini.

Judith Ngussa Kuungana na Millen

Mrembo wa Tanzania katika mashindano ya Miss Universe 2024, Judith Ngussa, amepongeza hatua ya Millen Magese kupewa leseni ya kuandaa mashindano hayo mwaka 2025, akiahidi kushirikiana naye bega kwa bega.

"Nimefurahishwa kuona dada Millen kuwa muandaaji wa Miss Universe Tanzania. Niko tayari kushiriki katika safari ya kumtafuta mwakilishi wetu wa 2025 na kuwasaidia warembo wanaojitokeza," amesema Judith.
2