Ajali ya ghorofa Kariakoo, serikali kutunga sheria udhibiti majengo

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 11:51 AM May 05 2025
Waziri wa Ujenzi Abdalah Ulega akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo leo bungeni Dodoma.
Picha: Ibrahim Joseph
Waziri wa Ujenzi Abdalah Ulega akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo leo bungeni Dodoma.

Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amesema serikali inaendelea na taratibu za kutunga sheria ya majengo itakayokuwa na jukumu la kusimamia sekta ya ujenzi, ili kutumika kama mwarobaini wa changamoto kama ajali ya ghorofa lililoporomoka Kariakoo, na kwamba itakuwa mahususi katika masuala ya uratibu, usimamizi na udhibiti sekta ya majengo nchini.

Ulega amebainisha hayo leo Mei 2024, Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka 2025/26, akieleza kuwa kutungwa kwa sheria hiyo ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kutokea kwa ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa nne katika eneo la Kariakoo Jijini Dar es salaam, Novemba 16, 2024 na kusababisha vifo, majeruhi pamoja na upotevu wa mali.

"Nitumie fursa hii kutoa pole kwa wote walioathirika kwa namna moja ama nyingine na maafa haya na ninawaombea marehemu wote wapumzike kwa amani," amesema Waziri Ulega.

Pia Waziri Ulega amemshukuru Rais Samia kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya ya kuliongoza Taifa, akisema watanzania wote ni mashuhuda wa namna alivyofanya mapinduzi makubwa katika sekta zote nchini.

Kadhalika ameeleza kuwa chini ya uongozi wa Rais Samia miradi mikubwa imetekelezwa, suala ambalo litasaidia kuchochea maendeleo katika sekta nyingine za kiuchumi na kijamii na hivyo kukuza uchumi wa mtu mmoja na Taifa kwa ujumla.

BUNGENI