Gwajima apiga marufuku 'vigoma' ndani ya daladala

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 02:09 PM May 05 2025
Daladala
Picha: Mtandao
Daladala

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, amekemea tabia ya baadhi ya wanawake wanaocheza ngoma maarufu 'kigoma' ndani ya daladala, kisha kuelekeza makalio yao madirishani.

Amesema tabia hiyo haidhalilishi tu utu wa wanawake nchini, bali inakwenda kinyume na maadili na kusababisha kizazi kinachokua kuharibiwa kimaadili.

Dk. Gwajima, kupitia ukurasa wake mtandaoni, amesema ameshuhudia baadhi ya video abiria wakicheza goma hiyo huku baadhi yao wakielekeza makalio madirishani.

"Nakemea vikali, wanaocheza ngoma ya ajabu isiyo na maadili kwenye basi la abiria lenye mwonekano kama kwenye picha hapo.

"Haya maadili tunayoyatamani kila siku kwamba, yawe yapo imara ili kudhibiti ukatili wa kijinsia, hayatafanikishwa na mtu mmoja au kiongozi mmoja bali, jamii yote kwa ujumla na mtu mmoja mmoja kwa nafasi yake.

"Haiwezekani watu wazima na akili zao wanakodi gari wanapiga ngoma wanawake kwa wanaume, huku ndani kuna watoto halafu mwanamke mmoja mtu mzima anacheza ngoma hiyo kwa staili ya aibu.

"Kama haitoshi anafungua dirisha, anavua nguo anabaki utupu, nusu ya mwili kuanzia kiunoni nje, anachezesha maungo na walio kwenye gari hilo wanashangilia pia walio nje wanashangilia halafu tuseme hapa tunapambana na mmomonyoko wa maadili, ili tudhibiti ukatili wa kijinsia.

"Wito kwa jamii, tuache haya mambo ya hovyo, hayafai na anayefanya hivi analeta maswali mengi kuhusu alivyoiva kwenye malezi na makuzi na pengine, zaidi ya hapo. 

"Aidha, mambo haya ya hovyo yanaharibu watoto wetu. Wito mahsusi kwa wanawake wanaofanya haya, tuache mambo haya kwani, yanadhalilisha utu wa wanawake wote na kurudisha nyuma vita ya kupambana kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake.

"Wito kwawanaume, tuache kushangilia mambo haya ya hovyo, tukemee vikali. Kwa mila na desturi njema za kitanzania, Wanaume wanayo nafasi kubwa kwenye kusimamia ulinzi na ustawi wa maadili chanya kwenye jamii.

"Wito kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri wa umma, tushirikiane kuwakabidhi Polisi abiria aina hii. Aidha, nadhani mmiliki wa basi hili la abiria hawa, tupe ushirikiano, ili hawa abiria ikiwezekana wajulikane kwa hatua zaidi."