Ukatili kosa la kumsimamisha mgombea, chama kufanya kampeni

By Salome Kitomari , Nipashe
Published at 10:05 AM Apr 19 2025
news
Mtandao
Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ramadhani Kailima.

Unyanyasaji au ukatili wa kijinsia ni moja ya kosa la kimaadili ambalo adhabu yake ni kukisimamisha chama cha siasa au mgombea kufanya kampeni kwa muda ambao kamati itaona unafaa au kulipa faini isiyopungua Sh. milioni moja au vyote.

Kanuni hizo zilizochapishwa kwenye Gazeti la Serikali kwa Tangazo Namba 249 Aprili 18,2025 zikiitwa za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025, ambazo zimeweka Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ngazi ya kata, jimbo na kitaifa.

Kamati inaweza kukisimamisha chama cha siasa au mgombea kuendelea kufanya kampeni za uchaguzi kadiri itakavyoonekana inafaa. 

”Kwa madhumuni ya aya hii, kuzuiwa kufanya kampeni za uchaguzi itajumuisha zuio la kufanya mikusanyiko ya aina yoyote inayoashiria kufanya kampeni za uchaguzi,”imefafanuliwa.

Pia kamati inaweza kuzuia chama cha siasa au mgombea kutumia vyombo vya habari au kubandika machapisho ya kampeni kwa muda ambao kamati itaona unafaa; na kukitaka chama cha siasa au mgombea kulipa faini.

Faini hizo ni ikiwa ni katika ngazi ya kata, kiasi kisichozidi Sh. 200,000 ambacho kitathibitishwa na kamati ya jimbo, na ikiwa ni katika ngazi ya jimbo, kiasi kisichozidi Sh. 700,000 ambacho kitathibitishwa na kamati ya kitaifa.

Aidha, ikiwa ni katika ngazi ya kitaifa, kiasi kisichozidi Sh. milioni 1.500,000 au kwa kadiri kamati itakavyoona inafaa.

Pia kanuni hizo zimeweka Mamlaka ya Kamati ya Rufaa ya Maadili ya Uchaguzi kuwa inaweza kuchukua hatua zifuatazo katika kushughulikia malalamiko kama kutoa onyo au karipio;kuagiza upande uliokiuka maadili kusahihisha kosa au makosa yaliyotendeka na iwapo italazimu kuuomba umma msamaha.

Pia kungaza jina la chama cha siasa au mgombea aliyekiuka maadili na kueleza kosa au makosa yake kwa njia ya taarifa kwa umma kupitia redio, televisheni, magazeti na njia nyingine za mawasiliano kama itakavyoonekana inafaa;

Vile vile, kamati inaweza kuelekeza malalamiko mengine kwenye mamlaka husika kama itakavyoona inafaa kwa hatua zinazostahili; kusimamisha chama cha siasa au mgombea kuendelea kufanya kampeni za uchaguzi kwa muda kama itakavyoona inafaa;

Aidha, kuelekeza chama cha siasa au mgombea kulipa faini isiyozidi Sh.700,000 kwa ukiukwaji wa maadili kwa uchaguzi wa ubunge na isiyozidi Sh. milioni 1.5 kwa uchaguzi wa urais au kwa kadiri kamati itakavyoona inafaa.

Vile vile, kamati itakuwiwa kuchunguza malalamiko yote yaliyowasilishwa kwa njia ya rufaa kabla ya kufanya maamuzi; faini zote zitakazotozwa katika kamati zote zitalipwa kupitia Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na zitakatiwa risiti.

Pia kamati ya rufaa inaweza kuitisha na kupitia uamuzi uliotolewa na kamati ya kitaifa na inaweza kukubaliana au kubadilisha uamuzi husika.