CCM Kilindi: Samia amemaliza yote, wote mtashinda

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:33 PM Apr 19 2025
Rajabu Kumbi Mwenyekiti wa CCM wilayani Kilindi
PICHA: MTANDAO
Rajabu Kumbi Mwenyekiti wa CCM wilayani Kilindi

MWENYEKITI CCM wilayani Kilindi, Rajabu Kumbi amewataka madiwani kuondoa hofu juu ya kurejea nafasi zao kwa maelezo kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa katika kufanikisha miradi ya maendeleo ya wananchi.


Kumbi ameyasema hayo leo Aprili 19,2025  alipokuwa akizungumza kwenye Mkutano wa robo ya tatu ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga akiwasisitiza wajumbe hao kuyasema yale yote mazuri yaliyotekelezwa na Rais Samia.

Amesema, katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, Rais Samia atapata kura nyingi zisizo kifani kutoka wilayani Kilindi kwa vile amepeleka fedha nyingi za utekelezaji wa miradi.

"Sisi Kilindi hatuna wasiwasi, wakati ukifika wala hatutasema sana sisi tutafanya kazi ya kuonyesha tu yale yaliyofanywa na Rais,ameleta fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo hivyo tuendelee kumsemea nasi tusihofu,"amesema Kumbi.

Kuhusu migogoro ya ardhi Wilayani Kilindi, amewataka madiwani kushirikiana na watendaji katika kutatua.

Amesema wakati jitihada mbalimbali zikiendelea kufanyika kuondosha migogoro hiyo ya ardhi madiwani wanapaswa kushiriki kikamilifu kumaliza changamoto hiyo akiwaasa kutokuwa chanzo cha tatizo husika.

Katibu wa CCM wilaya ya Kilindi, Asha Jumanne


"Niwaombe ndugu zangu kwenye maeneo yetu tukashirikiana kutatua migogoro ya ardhi na kamwe tusiwe chanzo cha migogoro hiyo,"amesema Kumbi akiasa Madiwani kutotumia uongozi wao kuwaomba Kura wananchi huku waliahidi kulipa fadhila kupitia ardhi zenye migogoro kugawa haki upande mmoja.

"Madiwani kama ni kura zije kwa kuondosha migogoro na isiwe kwa kuiongeza,"amesema.

Naye, Katibu CCM Wilayani Kilindi, Asha Jumanne Mwendwa amewataka madiwani na watumishi wengine kumpatia ushirikiano ili kuiwezesha serikali kuhamasisha maendeleo.

Amesema kuwa, suala la ushirikiano lina umuhimu wa kipekee kwenye uharakishaji wa maendeleo ya Wananchi na kwamba kwa vile watendaji wa CCM na wale wa serikali nia yao ni moja hakuna sababu kukwazana.

"Sisi wote tunajenga nyumba moja kwanini tugombee fito? naomba tushirikiane ingawa hapa ni mgeni ila kikazi sio na nimemuona mmoja wa watumishi nilikuwa naye Lindi,"amesema Katibu huyo wa CCM.