Serikali yashauriwa kushirikiana na wananchi kulinda barabara

By Christina Haule , Nipashe
Published at 02:19 PM Apr 19 2025
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka akiwa kwenye mstari wa pamoja na viongozi wengine wa chama na serikali baada ya mkimbiza Mwenge wa uhuru kitaifa Ismail Ali Ussi  kuziindua barabara ya Ruaha kona wilayani humo.
PICHA: CHRISTINA HAULE
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka akiwa kwenye mstari wa pamoja na viongozi wengine wa chama na serikali baada ya mkimbiza Mwenge wa uhuru kitaifa Ismail Ali Ussi kuziindua barabara ya Ruaha kona wilayani humo.

SERIKALI imeshauriwa kushirikiana na jamii kujenga tabia ya kusafisha mitaro ya pembezoni mwa barabara mara kwa mara ili kuondokana na uharibifu wa barabara na kudai matengenezo mapema yanayorudisha nyuma kasi ya maendeleo ya nchi.

Mkimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa 2025 Ismail Ali Ussi amesema hayo leo wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara yenye urefu wa Kilometa 400 iliyojengwa kwa kiwango cha lami na nusu yake zege katika eneo la Ruaha Wilayani Kilosa mkoani hapa.

Ussi anasema miundombinu ya barabara inapaswa kulindwa sababu serikali inatumia fedha  katika matengenezo na inapotokea barabara kuharibika hulazimisha fedha nyingine kuingia kwenye mradi huohuo na kufanya miradi mingine kuendelea kusubiri.

Akisoma taarifa  ya mradi kutoka Wakala wa barabara za vijijini na Mijini (TARURA) Kilombero Mhandisi Nurdin Msengi kwa niana ya Meneja wa Wilaya Kilombero Sadick Karume anasema barabara hiyo inajengwa kwa Kilometa 210 kiwango cha lami na Kilometa 200 kiwango cha zege kwa gharama ya shilingi Milioni 499.9 ambapo utekelezaji wake ulikamilika tangu Februari 2025.

Anasema mradi huko.utachochea ukuaji wa eneo la Mkamba mradi ulipo kwa kuongeza wigo wa biashara, kuboresha usafiri na usafirishaji kwa kuwa ni kiunganishi kikubwa cha kituo CHA treni ya abiria na kiwanda cha sukari cha Kilombero.

Mwenge wa Uhuru pia uliweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara Ruahakona ambapo Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro Mhandisi Juliana Masaro alisema ujenzi wa  barabara ya RuahaKona - Kilombero II yenye urefu wa Kilometa 0.71 kiwango cha zege umegharimu shilingi Milioni 949.3.


Mhandisi Masaro alisema malengo ya mradi huo ni kusaidia wananchi wanaotumia barabara hiyo inayounganisha kiwanda cha sukari Kilombero (K2) na barabara ya Mikuki- Ifakara wapate huduma Bora ya miundombinu ya usafiri na usafirishaji