UVCCM wahitimisha ziara ya “Mama Full Box Oparesheni”

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 06:20 PM Apr 18 2025
UVCCM wahitimisha ziara ya “Mama Full Box Oparesheni”, wasisitiza uchaguzi upo pale pale
Picha: Marco Maduhu
UVCCM wahitimisha ziara ya “Mama Full Box Oparesheni”, wasisitiza uchaguzi upo pale pale

Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini leo imehitimisha rasmi ziara ya Mama Full Box Oparesheni, kwa kufanya mikutano ya hadhara katika Kata za Ibinzamata na Kitangili, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha wananchi kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Akizungumza wakati wa hitimisho hilo, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya hiyo, Abdulaziz Sakala, alisema vijana wameguswa na kazi kubwa aliyoifanya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, ikiwemo utekelezaji wa miradi ya kimkakati na maendeleo kwa wananchi.

“Ndugu zangu, Rais Samia ndani ya miaka minne ya dhahabu amefanikisha miradi mikubwa kama Daraja la Busisi, Bwawa la Mwalimu Nyerere, Reli ya SGR, na hapa Shinyanga tumeona ujenzi wa Uwanja wa Ndege. Tunataka aendelee kuongoza – Mitano Tena,” alisema Sakala.

Kwa upande wake, Katibu wa UVCCM Wilaya hiyo, Naibu Katalambula, aliwahimiza wananchi kujiandaa na kushiriki uchaguzi kwa mujibu wa Katiba, huku akiwataka wapigie kura wagombea wa CCM kuanzia ngazi ya Udiwani, Ubunge hadi Urais.

“Tutaendesha kampeni zetu kwa amani. Vijana na wananchi wote tunapaswa kupuuza propaganda za baadhi ya vyama vya upinzani vinavyolenga kuvuruga amani. Tuendelee kuiunga mkono Serikali yetu,” aliongeza Katalambula.

Diwani wa Ibinzamata, Ezekiel Sabo, alipongeza juhudi za UVCCM kueneza ujumbe wa maendeleo na kusema kuwa utekelezaji wa Ilani ya CCM umefikia asilimia 85 katika kata hiyo, huku miradi mingi ikiwa ni masoko na stendi ya kisasa ya mabasi.

Naye Diwani wa Kitangili, Mariamu Nyangaka, alisema kata yake imepiga hatua kubwa katika miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, ikiwemo ujenzi wa barabara, madaraja na zahanati mpya.

Ziara hiyo ya Mama Full Box Oparesheni ilianza Aprili 5, 2025 na imehitimishwa leo Aprili 17, 2025, ikiwa ni sehemu ya kampeni za kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

🟢 Kauli mbiu yao: “Kazi na Utu, Tunasonga Mbele.”

WATOTO.jpg 1.74 MB