Waziri wa Maji Juma Aweso, amepiga marufuku Mamlaka za Maji Safi na Usafi wa Mazingira nchini kuwakatia huduma wateja wenye madeni ya maji siku za mwisho wa wiki na sikukuu.
Alipiga marufuku hiyo juzi alipofanya ziara ya kukagua miradi ya uchimbaji visima vya maji jijini Dodoma pamoja na mradi wa kimkakati wa maji wa miji 28 uliopo wilayani Chamwino mkoani hapa.
Alisema ni marufuku kwa watumishi wa wizara hiyo kusitisha huduma ya maji kwa wateja wanaodaiwa ankara za maji katika siku za mwisho wa wiki na sikukuu.
“Watumishi wa Wizara ya Maji ni marufuku kumkatia maji mtu siku ya ‘weekend’ ama sikuku unakuta watu wamepumzika na familia zao mara huduma ya maji inakatwa ni marufuku kuanzia sasa na haya ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema.
Aidha, alitoa maelekezo kwa mkandarasi Megha Engineering, anayetekeleza mradi wa maji wa miji 28, wilayani Chamwino kufanya kazi usiku na ili kukamilisha kwa wakati.
“Mradi huu fedha tayari zimetolewa na kwa mujibu wa mkataba hadi sasa mkandarasi alipaswa kuwa amefika asilimia 70 ya utekelezaji wake lakini yupo asilimia 15 hivyo anapaswa kufanya kazi usiku na mchana ili kufikia matakawa ya mkataba, msimamizi wa mradi unapaswa kumsimamia vinginevyo nitakuondoa wewe,” alisema.
Mbunge wa Chamwino na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi, alisema wanaishukuru serikali kwakuwa mradi huo utamaliza tatizo la mgawo wa maji.
Hata hivyo, alisema mahitaji ya maji kwa siku katika wilaya hiyo ni lita milioni 7.5 wakati uzalishaji ni lita milioni 4.8, hivyo kufanya upungufu kuwa lita milioni 2.7.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED