Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeweka wazi barua ya Februari 20,2025 yenye kumbukumbu C/HQ/ADM/SG/02 waliyomjibu mwanachama wake, Lembrus Mchome, kwamba Baraza Kuu Taifa la chama hicho, lilikuwa halali na akidi ilitimia.
Katika barua hiyo yenye kichwa cha habari cha Malalamiko ya kuthibitishwa/kupitishwa kwa viongozi kinyume na katiba ya chama, imesainiwa na Katibu Mkuu, John Mnyika, akijibu barua yenye Kumb. Na. KM/CDM/A-B/2025 ya Februari 18, 2025.
Chama hicho kimejibu hoja nane za Mchome kwamba hoja sababu zote nilizozitaja hapo juu, malalamiko na maombi yako yote hayana ukweli wala msingi wowote.
Hoja za Mchome ni kwamba idadi ya wajumbe halali wa Baraza Kuu waliohudhuria kikao hicho ni 234, ambayo ni sawa na asilimia 56.8 ya wajumbe wote; Kwamba kwa mujibu wa Katiba yetu ya Chama ibara ya 6.2.2(a), kikao halali cha ngazi ya kawaida, kama vile Baraza Kuu, kinahitaji akidi ya asilimia 50 ya wajumbe wote wa kikao hicho;
Kwamba, kikao halali cha maamuzi ya kisera, au cha uchaguzi, au cha kurekebisha Katiba ya Chama, kama vile Mkutano Mkuu wa Chama Taifa, kinahitaji akidi ya asilimia 75 ya wajumbe wote wa kikao hicho;
Kwamba. Kikao cha Baraza Kuu unachokilalamikia hakiwezi kuwa kikao cha maamuzi ya kisera au kikao cha uchaguzi au cha kubadilisha Katiba bali kilikuwa kikao cha kawaida cha Baraza Kuu kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya kawaida ya Baraza Kuu yaani kuthibitisha jina la Katibu Mkuu, Manaibu Katibu Wakuu na wajumbe wa Kamati Kuu walioteuliwa na Mwenyekiti wa Chama:
Kwamba, Lilian Masiaga na Injinia Dk. Nyamatari Tengecha, unaodai walikuwepo ndani ya ukumbi wa kikao cha Baraza Kuu sio wajumbe na hawapo kwenye orodha ya mahudhurio ya wajumbe wa Baraza Kuu.
“Kwa hiyo kuwepo au kutokuwepo kwao hakuwezi kuathiri akidi ya kikao cha Baraza Kuu wala kubatilisha maamuzi yaliyofanyika katika kikao tajwa,”amejibu.
Kwamba, kwa mujibu wa kumbukumbu za kikao cha Baraza Kuu unachokilalamikia, wewe mwenyewe hukuhudhuria kikao hicho.
“Kwa hiyo, inaelekea malalamiko yako yametokana na maneno ya kuambiwa ama ya kuhisi, lakini yasiyokuwa na ukweli au msingi wowote,”amefafanua Mnyika kwenye barua hiyo.
“Ingependeza sana kama mwanachama na kiongozi wa chama kama ungetafuta ukweli wa jambo hili kwenye ofisi yangu kwanza kabla ya kuandika na kusambaza uzushi huu mitandaoni na kwenye vyombo vya habari na hivyo kuleta taharuki ya bure kwa wanachama na wananchi,”amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED