Aliyekuwa Mbunge wa Mlimba, Suzan Kiwanga, viongozi wengine watatu na wanachama 50 wa Wilaya za Kilosa na Kilombero na wanachama 50 mkoani Morogoro wametangaza kuondoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Mbali na Suzan ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (BAWACHA), wengine ni Mwenyekiti wa BAWACHA Wilaya ya Kilombero, Magreth Lipindi, Mwenyekiti wa BAVICHA Wilaya ya Kilosa, David Chiduo, ambaye pia aliyewahi kuwa Diwani wa Kata ya Viwanja Sitini na aliyekuwa Mwenyekiti wa BAWACHA Wilaya ya Kilosa, Sheila Mkubwa.
Viongozi hao wametangaza uamuzi huo leo Mei 13,2025, wakieleza sababu kubwa ni msimamo wa CHADEMA kutoshiriki Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, wakiendelea kushikilia msimamo wa ‘No Reforms No Election’.
Aidha, wamesema mwenendo wa viongozi wa chama hicho siw a kuridhsiha na kwamba wamekijenga kwa nguvu kubwa kwa kutembea maeneo mbalimbali kwa gari na miguu, ikiwamo kujitolea mali na muda wao.
Kwa mujibu wa Suzan, tangu kumalizika kwa uchaguzi wa CHADEMA Januari 22, 2025, amekuwa akipokea jumbe za matusi, kejeli na manyanyaso akiitwa msaliti mambo ambayo yanayotweza utu wake, na kutothamini mchango wake ndani ya chama hicho.
“Tumepata changamoto nyingi sana. Baada ya Uchaguzi Mkuu wa ndani ya chama. Uchaguzi ulivyoisha tulitegemea kiongozi ambaye yupo madarakani mpaka hivi sasa, Mheshimiwa Lissu hakuweza kabisa kutuunganisha sisi wanachama,”amesema Suzan.
"Kama hatutashiriki uchaguzi, hatutakuwa na wagombea wa ubunge, udiwani, wala urais. Na tunapouliza au kuhoji kuhusu uamuzi huu, tunawekewa alama ya usaliti na kuitwa 'timu Mbowe' kana kwamba kuwa na mtazamo tofauti ni kosa.Sasa kama chama bila mabadiliko hakiwezi kushiriki uchaguzi na mimi niliingia CHADEMA kwa sababu nina malengo ya kuwasaidia wananchi wangu wa eneo langu ambao wanateseka maana yake hilo duka limefungwa mlango.
“Kwa hiyo mimi ndoto zangu na ndoto za CHADEMA ni vitu viwili tofauti. Sasa leo tunahamasishwa tukapambane tukazuie uchaguzi. Lissu familia yake iko Ulaya. Mke wake Lissu yuko Ubelgiji, wanaye Lissu wapo Marekani. Wamechukua uraia wa Marekani,”David Chiduo, aliyekuwa mwenyekiti CHADEMA Kilosa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED