Rais wa Finland kuzuru Tanzania

By Salome Kitomari , Nipashe
Published at 07:45 PM May 13 2025
Rais wa Jamhuri ya Finland, Alexander Stubb.
Picha:Mtandao
Rais wa Jamhuri ya Finland, Alexander Stubb.

Rais wa Jamhuri ya Finland, Alexander Stubb, anatarajia kufanya ziara ya kitaifa nchini Tanzania kuanzia Mei 14 hadi 16 Mei, 2025, kwa mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Taarifa kwa umma iliyotolewa leo Mei 13,2025 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais-Ikulu, imeeleza kuwa viongozi hao wanatarajia kufanya mazungumzo ya pamoja na kuzungumza na waandishi wa habari. 

Aidha, katika ziara hiyo, Rais huyo atakuwa na matukio mbalimbali ikiwemo kushiriki katika semina kuhusu Urithi wa Hayati Martti Ahtisaari, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Finland na mwanadiplomasia mbobezi aliyeshika nafasi mbalimbali ikiwemo Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Namibia na Kosovo na pia aliwahi kuwa Balozi wa Finland nchini Tanzania.

Mbali na viongozi wa kiserikali, Rais Stubb pia ameambatana na wafanyabiashara kutoka nchini Finland ambapo atahutubia katika jukwaa la wafanyabiashara wa Tanzania na Finland linalotarajiwa kufanyika Mei 16, 2025 ili kujadili fursa za kiuchumi na biashara baina ya nchi hizi mbili.

Aidha, jukwaa la wafanyabishara litakuwa chachu ya kuchochea biashara na uwekezaji baina ya nchi hizi mbili ambapo Tanzania inategemea kunufaika na mitaji na uwekezaji kutoka Finland.

“Finland na Tanzania zina mahusiano ya miaka 60 na zimekuwa zikishirikiana katika sekta za elimu, misitu, mageuzi kwenye mifumo ya kodi, usawa wa kijinsia na maeneo mapya ya mabadiliko ya tabianchi, ulinzi, uchumi wa buluu, akili mnemba na TEHAMA,”imefafanua taarifa hiyo.