Serikali yatenga zaidi ya sh. bilioni 207 kulipa madai ya wastaafu

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 07:56 PM May 13 2025
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu.
Picha: Mtandao
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu.

Serikali imesema zaidi ya Sh. bilioni 207 zimetengwa kwa mwaka wa fedha 2024/25 kwa ajili ya kulipa madai ya wastaafu ambayo bado hayajalipwa.

Aidha, waajiri wote wametakiwa kuwasilisha taarifa za wastaafu wenye madai yao mapema, ili kuwezesha Hazina kushughulikia na kulipa madai hayo bila kuchelewa.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu ametoa kauli hiyo  leo bungeni alipokuwa akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Rita Kabati.

Katika swali lake, Mbunge huyo ametaka kujua hatua za serikali dhidi ya waajiri wanaochelewesha malipo kwa watumishi wa umma waliopandishwa vyeo na baadaye kustaafu.

Sangu ameeleza kuwa serikali imejipanga kikamilifu kushughulikia suala hilo, na tayari Sh bilioni 2.7 zimelipwa kwa watu 1,200 waliokuwa na madai hayo katika mwaka wa fedha 2024/25.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Nyasa (CCM), Stella Manyanya ametaka kujua lini serikali italipa stahiki za wastaafu waliopandishwa vyeo lakini utekelezaji wa nyongeza hizo za vyeo ulisitishwa.

Naibu Waziri Sangu amesema suala hilo linawahusu watumishi waliopandishwa vyeo na taarifa hizo kuingizwa kwenye mfumo wa malipo kabla ya mchakato wa uhakiki kusitisha utekelezaji wake Juni 2016 na baadhi ya watumishi hao walistaafu kabla ya vyeo hivyo kurejeshwa rasmi Novemba 2017.

Hata hivyo, Sangu alimehakikishia Bunge kuwa wastaafu hao watalipwa mshahara wao unaotokana na vyeo walivyopandishwa kuanzia tarehe ya kupandishwa hadi tarehe ya kustaafu.
Amefafanua kuwa malipo hayo yanafanyika kupitia kwa waajiri wa zamani wa wastaafu husika.