Mwenyekiti CCM Bagamoyo akoshwa usimamizi miradi Chalinze

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 05:17 PM May 13 2025
 Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo, Abubakary Mlawa.
Picha: Julieth Mkireri
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo, Abubakary Mlawa.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo, Abubakary Mlawa, amepongeza usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Chalinze na kuzitaka mamlaka husika kuongeza ubunifu katika kubuni vyanzo vipya vya mapato.

Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika mjini Chalinze, Mlawa amesema utekelezaji wa miradi hiyo umewezekana kutokana na Serikali kuidhinisha fedha kwa wakati pamoja na usimamizi thabiti wa mapato ya ndani, hali iliyowezesha kutatua changamoto za wananchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali.

“Kazi nzuri inayofanywa ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya CCM katika kuwahudumia wananchi. Na mimi katika kipindi changu cha uongozi, nitasimamia kikamilifu utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa ufanisi, uwazi na kushirikisha wananchi,” amesema Mlawa.

Aidha, ametoa onyo kali kwa wataalamu wa halmashauri hiyo kuacha mara moja kushiriki kwenye uuzaji holela wa mashamba, akisema kitendo hicho kimekuwa chanzo cha migogoro ya ardhi. Alisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kuhusika, ikiwemo viongozi wa chama.

1

“Mtaalamu au kiongozi yeyote atakayehusika na uuzaji holela wa mashamba hatavumiliwa. Sitamfumbia macho hata kama ni kiongozi wa chama; sheria ichukue mkondo wake,” ameongeza.

Katika kuelekea uchaguzi, Mlawa aliwataka madiwani wote kuwa waadilifu na kutekeleza majukumu yao kwa weledi, akisisitiza kuwa chama hakiwezi kumpitisha mgombea yeyote atakayekiuka maadili.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Bagamoyo, Faiswal Hamadi, amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze, Ramadhani Possi, kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kutumia fedha za mapato ya ndani na za serikali kuu.

2