Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imekilima barua Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akiwataka waitishe kikao kingine cha Baraza Kuu la Taifa kujaza nafasi za viongozi zilizokuwa wazi kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za CHADEMA.
Aidha, ameelekeza baada ya kukamilisha hilo chama hicho kiwasilishe taarifa kwake (msajili) kwa mujibu wa sheria.
Taarifa ambayo Nipashe Digital imezipata leo Mei 13,2025 zinaeleza kuwa msajili amefanya uamuzi huo baada ya kupokea malalamiko ya mwanachama wa CHADEMA, Lembrus Mchome ya Machi 15 Machi 2025 kulalamika uhalali wa kikao chenu cha Baraza Kuu la Taifa cha Januari 22, 2025.
Zinaeleza kuwa Msajili amefanyia kazi malalamiko na kubaini kuwa malalamiko yake ni ukweli kwamba kikao cha Baraza Kuu la Taifa la CHADEMA kilichofanyika Januari 22, 2025 kilikuwa batili, kwa sababu kilikuwa hakina akidi inayotakiwa kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA ya Mwaka 2006 toleo la 2019.
Aidha,amesema hata kama kikao hicho kingekuwa halali, uthibitishaji viongozi uliofanywa na kikao hicho ulikuwa batili, kwa sababu watu ambao siyo wajumbe wa kikao hicho walikuwa ndani ya ukumbi na baadhi walipiga kura.
Viongozi wanaolalamikiwa kuwa walithibitishwa na Baraza Kuu la CHADEMA Taifa ambalo Msajili anasema ni batili, ni pamoja na Katibu Mkuu John Mnyima, Naibu Katibu Mkuu Bara Aman Golungwa, Naibu Katibu Zanzibar, Ali Ibrahim Juma.
Wengine ni Wajumbe wa Kamati Kuu Godbless Lema, Rose Mayemba, Dk. Rugemeleza Nshala, Salima Kasanzu na Hafidh Ali Saleh.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED