Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, umekabidhi madawati 100 kwa shule mbili za msingi ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya ujifunzaji kwa wanafunzi na kuondoa changamoto ya kukaa chini wakati wa masomo.
Madawati hayo yalitolewa rasmi leo na Mhifadhi Mwandamizi wa TFS, Ester Msokwa, kwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama,Mboni Mhita, katika hafla iliyofanyika katika Shule ya Msingi Wendele, kata ya Wendele, Manispaa ya Kahama. Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na wazazi pamoja na wananchi wa eneo hilo.
Akizungumza katika makabidhiano hayo, Msokwa alisema kuwa TFS imetoa madawati hayo 100, ambapo 50 yamepelekwa katika Shule ya Msingi Igwamanoni iliyopo Halmashauri ya Ushetu na mengine 50 katika Shule ya Msingi Wendele. Amesisitiza kuwa msaada huo ni sehemu ya mpango endelevu wa TFS kusaidia sekta ya elimu kila mwaka.
“Tunalenga kupunguza changamoto ya uhaba wa madawati katika shule zetu. Tunatoa wito kwa uongozi wa shule na wanafunzi kuyatunza madawati haya ili yaweze kuwasaidia wanafunzi wa sasa na wa baadaye,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Msingi Wendele, Gasto John, ameeleza shukrani kwa kupokea msaada huo, akibainisha kuwa shule sasa imepata ziada ya madawati 20 kwani mahitaji yake yalikuwa madawati 272. Aliahidi kuwa uongozi wa shule utayatunza vyema ili yawe na manufaa ya muda mrefu.
Akizungumza baada ya kupokea madawati hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, ameipongeza TFS kwa mchango wake katika kuboresha mazingira ya elimu wilayani humo. Alisema serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa, maabara na ukarabati wa madarasa chakavu.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi wanaoishi karibu na misitu inayosimamiwa na TFS kushirikiana na wakala huo katika kuitunza, kwani misitu hiyo ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya jamii, kama inavyoonekana kupitia msaada huu wa madawati. Aliwahimiza pia kuwa wakali kwa wale wote wanaobainika kuharibu misitu hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED