Miradi 80 kutekelezwa kwa muundo wa PPP

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 05:27 PM May 13 2025
Naibu Waziri Hamad Hassan Chande.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri Hamad Hassan Chande.

Wizara ya Fedha imesema hadi Aprili 2025, miradi 80 imewezeshwa kupitia utaratibu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), ikiwa ni katika kuimarisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati kwa kushirikiana na wawekezaji.

Naibu Waziri Hamad Hassan Chande ametoa kauli hiyo leo Mei 13,2025 bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM), Oran Njeza aliyetaka kufahamu miradi iliyotekelezwa kwa mfumo huo.

Akijibu swali hilo, Chande amesema utekelezaji wa miradi hiyo unafanyika chini ya mwongozo wa Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Sura ya 103, kifungu cha 10A cha sheria hiyo kilianzisha Mfuko wa Uwezeshaji wa Ubia (PPP Facilitation Fund – PPPFF) kwa ajili ya kusaidia maandalizi na utekelezaji wa miradi hiyo.

Amesema Kifungu cha 5(1) kimekipa Kituo cha Ubia (PPPC)  mamlaka ya kutoa usaidizi wa kiufundi kwa mamlaka za serikali na sekta binafsi katika hatua zote za uibuaji, maandalizi na utekelezaji wa miradi.

Naibu Waziri huyo amesema kati ya miradi 80 iliyowezeshwa na serikali, mitatu ipo katika hatua ya utekelezaji, minne ipo katika hatua ya majadiliano, miwili ipo katika hatua ya ununuzi, miradi 26 ipo katika hatua ya upembuzi yakinifu, miradi 13 ipo katika upembuzi yakinifu wa awali na miradi 32 ipo katika hatua ya maandalizi ya andiko dhana.

Katika swali la nyongeza, Njeza ametaka kufahamu mikakati ya serikali katika kutekeleza miradi yenye mvuto wa PPP hasa barabara ya Igawa–Tunduma, akieleza kuwa sheria ya bajeti inakataza serikali kutenga fedha kwa miradi hiyo, hivyo ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu.

Pia,amehoji hatua zinazochukuliwa na serikali kuhakikisha ujenzi na uendeshaji wa reli mpya ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) unatekelezwa kwa ushirikiano na sekta binafsi.

Akijibu hoja hizo, Naibu Waziri Chande amesema serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya PPP kwa kushirikisha sekta binafsi tangu hatua za awali.

Ameeleza kuwa tayari kuna mshiriki wa sekta binafsi anayeshughulikia maandalizi ya mradi wa barabara ya Igawa–Tunduma kupitia utaratibu wa PPP.

Kuhusu reli ya Tazara, Chande amesema Tanzania na Zambia zipo kwenye majadiliano ya pamoja na Serikali ya China na tayari wamefikia hatua nzuri.

Amebainisha kuwa serikali hizo ziko mbioni kusaini mkataba na mkandarasi kutoka kampuni ya China CECC kwa ajili ya kuanza kazi ya uboreshaji wa reli hiyo, jambo linaloashiria dhamira ya dhati ya serikali kushirikisha sekta binafsi katika miundombinu mikubwa ya kikanda.