ACT- Wazalendo waingia anga za CCM Geita Mjini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:19 PM May 13 2025
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwanachama wa ACT-Wazalendo,Innocent Charles, leo amechukua rasmi fomu ya kugombea ubunge wa Jimbo la Geita Mjini katika uchaguzi mkuu ujao, hatua inayotajwa kuwa ni sehemu ya mwamko mpya wa kisiasa unaolenga kuleta mabadiliko ya kweli nchini.

Mwanachama wa ACT-Wazalendo,Innocent Charles, leo amechukua rasmi fomu ya kugombea ubunge wa Geita Mjini katika uchaguzi mkuu ujao, hatua inayotajwa kuwa ni sehemu ya mwamko mpya wa kisiasa unaolenga kuleta mabadiliko ya kweli nchini.

Fomu hiyo alikabidhiwa na Katibu wa Jimbo la Geita Mjini, Paul Lwege, katika hafla iliyoambatana na ujumbe mzito wa matumaini, mabadiliko na kudai demokrasia ya kweli. Akizungumza mara baada ya kumkabidhi fomu, Lwege amesema hatua ya Charles ni ushahidi kuwa Watanzania wengi, sasa wana ujasiri wa kuingia kwenye uwanja wa siasa ili kuleta mabadiliko kutoka ndani ya mfumo uliopo.

“Tunashiriki uchaguzi si kwa sababu mfumo ni wa haki, bali kwa sababu tunaamini katika mapambano ya kudai mabadiliko kutoka ndani ya mfumo huo huo,” amesema Lwege.

Kwa kuchukua fomu hiyo, Innocent Charles anaungana na maelfu ya Watanzania wanaotafuta fursa ya kujenga taifa lenye misingi ya haki, usawa na demokrasia. Chama cha ACT-Wazalendo kimekuwa mstari wa mbele kudai marekebisho ya sheria za uchaguzi, kikisisitiza kuwa mfumo uliopo kwa sasa unalindwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa maslahi ya kisiasa.

Charles amesema dhamira yake ni kuwa sauti ya wananchi wa Geita Mjini, akiahidi kusimamia haki, maendeleo ya kweli na uwajibikaji kwa kila kiongozi aliyepewa dhamana na wananchi.

“Nagombea si kwa sababu nataka madaraka, bali kwa sababu nataka mabadiliko yenye tija kwa wananchi. Ni wakati wa siasa zenye heshima, uwazi na zinazojibu matatizo halisi ya wananchi,” amesema Charles baada ya kuchukua fomu.

ACT-Wazalendo inaendelea kuwahamasisha Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi, kulinda kura zao, na kujiunga na mapambano ya amani ya kudai mfumo wa uchaguzi wenye usawa na haki kwa wote.