MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Heche amesema wanaendelea kuwatambua viongozi walioteuliwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu licha ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutangaza kutokuwatambua.
Akiongea na wananchi wilayani Tarime mkoani Mara jana, Heche amesema hawatabadili chochote katika kile kilichofanywa na Mwenyekiti wao hata ikibidi kufutwa chama.
“Mimi nakwambia Msajili wewe huhitaji kumtambua Katibu Mkuu wa chama chetu sisi tunamtambua, wamewapa fedha watu wajifanye wanajitoa kwenye CHADEMA sasa hiyo CHADEMA wanayojitoa watu ndiyo hawa hapa hiyo nayo imeshindikana” amesema Heche.
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeitaka CHADEMA, kuitisha kikao kingine cha Baraza Kuu la Taifa kujaza nafasi za viongozi zilizokuwa wazi kwa sababu kilichofanyika Januari 22 mwaka huu ni batili.
Hiyo ni baada ya Ofisi ya Msajili kupokea malalamiko ya mwanachama wa CHADEMA, Lembrus Mchome ya Machi 15 mwaka huu, akilalamikia uhalali wa kikao hicho.
Wanaolalamikiwa kuwa walithibitishwa na Baraza Kuu la CHADEMA Taifa ambalo Msajili anasema ni batili, ni pamoja na Katibu Mkuu, John Mnyima, Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Aman Golungwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Ali Ibrahim Juma.
Wengine ni wajumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema, Rose Mayemba, Dk. Rugemeleza Nshala, Salima Kasanzu na Hafidh Ali Saleh.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED