Tanzania yazalisha tani zaidi ya milioni 10 za saruji 2024 – Waziri Jafo

By Ibrahim Joseph , Nipashe
Published at 02:29 PM May 14 2025
Waziri wa Viwanda na Biashara,Dk. Seleman Jafo.
Picha: Ibrahim Joseph
Waziri wa Viwanda na Biashara,Dk. Seleman Jafo.

Waziri wa Viwanda na Biashara,Dk. Seleman Jafo, amesema kuwa uzalishaji wa saruji nchini kwa mwaka 2024 umefikia tani 10,929,567.60, huku mahitaji ya ndani yakiwa ni takriban tani 8,500,000 kwa mwaka.

Dk. Jafo aliyasema hayo leo, Mei 14, 2025, wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2025/2026, katika kikao cha Bunge linaloendelea jijini Dodoma.

Ameeleza kuwa kiwango hicho cha uzalishaji kimezalisha ziada ya tani 2,429,567.60, ambazo huuza katika masoko ya nje ya nchi zikiwemo Rwanda, Malawi, Msumbiji, Burundi, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zambia.

Waziri Jafo amevitaja viwanda vinavyoongoza kuuza saruji nje ya nchi kuwa ni pamoja na:

  • 📌Dangote Industries Ltd


  • 📌Tanzania Portland Cement PLC


  • 📌Lake Cement Co. Ltd


  • 📌Mbeya Cement Co. Ltd


  • 📌Tanga Cement PLC

Aidha, amebainisha kuwa sekta ya uzalishaji wa saruji imechangia kwa kiasi kikubwa katika kutoa ajira nchini, ambapo jumla ya ajira 12,500 zimetolewa kupitia sekta hiyo. Kati ya ajira hizo, 5,220 ni ajira za moja kwa moja na 17,280 ni ajira zisizo za moja kwa moja.

Dk. Jafo amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya viwanda ili kuongeza uzalishaji, ajira na mchango wa viwanda katika pato la taifa.