Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima Wilaya ya Tunduru (TAMCU), Mussa Manjaule, ametoa wito kwa wakulima wa zao la korosho kujitokeza kwa wingi katika vituo maalumu vya ugawaji wa viuatilifu na dawa ili waweze kuzipokea kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa upuliziaji wa mikorosho katika mashamba yao.
Akizungumza na vyombo vya habari, Manjaule amesema ugawaji wa pembejeo hizo umeanza rasmi leo Mei 14, 2025, muda mfupi baada ya TAMCU kupokea tani 2,000 za pembejeo kwa ajili ya kuzisambaza kwa wakulima wa korosho wilayani humo. Alisema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha kuwa wakulima wanafanya maandalizi mapema ili kuongeza uzalishaji wa korosho msimu huu.
“Tunawaomba wakulima wote wa korosho kujitokeza mapema kwenye vituo vilivyopangwa ili wapokee pembejeo kwa wakati. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa msimu wa upuliziaji unaanza mapema na kwa ufanisi ili kuimarisha mavuno ya wakulima,” amesema Manjaule.
Aidha, Manjaule amesisitiza umuhimu wa wakulima kutambua kuwa sekta ya kilimo cha korosho ni miongoni mwa sekta muhimu kwa uchumi wa taifa, hasa katika kuingiza fedha za kigeni. Amesema wakulima wa zao hilo wanapaswa kutembea kifua mbele kwa mchango mkubwa wanaoutoa kwa taifa kupitia kilimo hicho.
Kwa mujibu wa Manjaule, TAMCU tayari imeagiza tani 60,000 za viuatilifu kwa ajili ya msimu huu wa upuliziaji, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuongeza uzalishaji. Alifafanua kuwa uzalishaji wa korosho umeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, ambapo msimu wa mwaka 2024/2025 umefikia tani 520,000, ukilinganishwa na tani 180,000 zilizozalishwa katika msimu wa 2022/2023.
Katika hatua nyingine, Manjaule aliwataka wakulima kuendelea na shughuli za usafi wa mashamba yao, ikiwa ni pamoja na kupalilia na kupanua mashamba kwa kupanda mikorosho ya kisasa ili kuongeza tija na kipato.
“Ni muhimu wakulima waachane na mashamba pori na waongeze ukubwa wa mashamba yao. Hii itaongeza uzalishaji, lakini pia kutengeneza fursa zaidi za kiuchumi kupitia sekta hii,” ameongeza.
Kadhalika, Mwenyekiti huyo alivitaka Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) kushirikiana na vyama vikuu katika kutoa elimu kwa wakulima juu ya mbinu bora za kuongeza uzalishaji na kushiriki katika mapinduzi ya viwanda vya ndani kwa ajili ya ubanguaji wa korosho, hatua itakayoongeza thamani ya mazao ya wakulima na kuongeza vipato vyao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED