Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imekabidhiwa boti 11 zenye thamani ya Shilingi milioni 539.834 kwa ajili ya kuimarisha juhudi za kudhibiti uvuvi haramu katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika mkoani Kigoma kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa, alisema boti hizo zitasaidia kuongeza ushiriki wa wavuvi katika kulinda na kusimamia rasilimali za uvuvi ili ziwe endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Boti hizo zimekabidhiwa kwa Serikali na Mradi wa Fish4ACP, unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na Serikali ya Ujerumani, na kutekelezwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) katika ukanda wa Ziwa Tanganyika.
“Matokeo haya ni sehemu ya juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza diplomasia ya uchumi kupitia ushirikiano wa kimataifa na washirika wa maendeleo, kwa lengo la kuinua kipato cha wananchi, kuimarisha usalama wa chakula na kuchochea uchumi wa jamii na taifa kwa ujumla,” alisema Rugwa.
Rugwa alieleza kuwa boti hizo zitakabidhiwa kwa vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMUs) vilivyopo katika maeneo ya Kibirizi (Manispaa ya Kigoma), Kagunga, Mtanga (Kigoma Vijijini), Mwakizega, Kabeba (Uvinza), Utinta, Kabwe (Nkasi), Samazi, Kipwa, Kasanga (Kalambo), pamoja na Kituo cha Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Kigoma (FRP).
Aidha, aliishukuru FAO kupitia Mradi wa Fish4ACP, pamoja na EU na Serikali ya Ujerumani, kwa msaada huo wa boti ambao unalenga kuimarisha ulinzi wa rasilimali za uvuvi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Mohamed Sheikh, alisema hali ya uvuvi nchini kwa sasa ni nzuri, na Serikali imeendelea kuimarisha biashara ya mazao ya uvuvi ndani na nje ya nchi.
Prof. Sheikh alisisitiza kuwa wizara itaendelea kusimamia ipasavyo rasilimali za uvuvi kwa manufaa ya wananchi na taifa, ikiwemo kulinda maeneo ya mazalia na makulio ya samaki kwa kutumia maboya maalum, sambamba na kudhibiti uharibifu wa mazingira.
Alibainisha pia kuwa katika kukabiliana na uvuvi haramu, Serikali imeanza kutumia teknolojia ya kisasa kwa kununua ndege nyuki (drones) ili kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa shughuli za uvuvi.
“Tayari Serikali imetoa boti 68 za doria, magari 20 na pikipiki 13 kwa vituo vya ulinzi wa rasilimali za uvuvi ili kuongeza ufanisi katika mapambano dhidi ya uvuvi haramu na kulinda mazalia ya samaki,” alisema Prof. Sheikh.
Aliwataka wavuvi wote kushirikiana na Serikali kwa kuacha kujihusisha na vitendo vya uharibifu wa rasilimali hizo muhimu na kushiriki kikamilifu katika juhudi za kutokomeza uvuvi haramu nchini.
Naye Mratibu wa Mradi wa Fish4ACP, Hashim Muumin, akizungumza kwa niaba ya Mwakilishi Mkazi wa FAO, alisema msaada huo wa boti ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi katika Ziwa Tanganyika, sambamba na utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Uvuvi na Mkakati wa Hiyari wa Usimamizi wa Uvuvi Mdogomdogo.
Muumin aliongeza kuwa msaada huo unalenga kuwawezesha wanavikundi vya BMUs kuendelea kushiriki kikamilifu katika ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi, hasa baada ya kupatiwa mafunzo mwaka uliopita.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED