Viongozi wa dini wilayani Ikungi, mkoa wa Singida, wamekitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhakikisha kinawateua wagombea wenye maadili, sifa stahiki na dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi kwa maendeleo ya Taifa.
Wito huo umetolewa leo Aprili 18, 2025, katika kikao kati ya viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali—ikiwemo CPCP, CCT, Wasabato, Kanisa Katoliki, BAKWATA, Cadria na Answar Sunna—na uongozi wa CCM wilayani humo.
Shekhe Rashid Galawa amesema hawana tatizo na CCM, lakini wanataka chama hicho kichague viongozi waadilifu, wenye hofu ya Mungu na nia ya kushirikiana na wananchi. Amesisitiza kuwa wakifanya hivyo, viongozi wa dini wako tayari kuwaunga mkono na kuwahamasisha waumini.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mchungaji Joseph Roche wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, ambaye amesema viongozi wa dini hutumika wakati wa uchaguzi tu, kisha kusahaulika hadi uchaguzi mwingine.
Mchungaji Mathayo Pinda ameelezea wasiwasi wake kuhusu wanasiasa wanaotoa ahadi hewa kwa waumini, jambo ambalo huwapa viongozi wa dini wakati mgumu mbele ya waumini wao.
Akijibu hoja hizo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ikungi, Mika Likapakapa, amesema chama kimepokea maoni hayo na kitaendelea kuyafanyia kazi kwa kuhakikisha wagombea wake wanazingatia maadili na matarajio ya wananchi.
Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Joshua Mbwana, amewataka viongozi wa dini kusaidia kutoa elimu ya amani kwa waumini wao, akisisitiza kuwa amani hiyo ndiyo msingi wa maendeleo na urithi wa viongozi waasisi wa Taifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED