TPDC kuunganisha gesi asilia nyumba zaidi ya 1,000 Dar

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 01:13 PM Apr 17 2025
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Dustan Kitandula.
Picha: Mtandao
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Dustan Kitandula.

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) lipo katika mpango wa kuunganisha gesi asilia katika nyumba zaidi ya 1,000 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kusambaza nishati safi ya kupikia majumbani.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Dustan Kitandula, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni (CCM), Abbas Tarimba, kwa niaba ya Waziri wa Nishati.

Katika swali lake la msingi, Mbunge Tarimba alitaka kufahamu hatua ambayo serikali imefikia katika utekelezaji wa mradi wa kusambaza gesi ya kupikia majumbani katika Wilaya ya Kinondoni.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Kitandula alieleza kuwa tayari serikali kupitia TPDC imepeleka miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia katika Wilaya ya Kinondoni, ambapo jumla ya nyumba 155 zimeunganishwa na mtandao wa matumizi ya gesi hiyo katika eneo la Mikocheni.

“Serikali kupitia TPDC ipo katika mpango wa kuunganisha nyumba zaidi ya 1,000 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, ambapo kati ya nyumba hizo, nyumba 279 zitapatikana katika Wilaya ya Kinondoni,” amesema Kitandula.

Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi, salama na rafiki kwa mazingira, sambamba na kupunguza matumizi ya mkaa na kuni ambazo zimekuwa na athari kwa misitu na afya za watumiaji.