WAKAZI wa Kijiji cha Lugala, kilichopo Kata na wilayani Malinyi, mkoani Morogoro, wameishukuru serikali, kwa kuwaondolea adha ya barabara ambayo awali ilisababisha hata vifo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Lugala, Erasto Mapuga, amesema hayo wakati Mwenge Uhuru kitaifa 2025 ulipozindua mradi wa barabara hiyo, na kwamba walikuwa wakipata shida kuvuka kwenye mto huo mkubwa hasa akinamama wajawazito na wagonjwa na wakati mwingine kufikia hatua ya kupoteza Maisha.
“Akinamama walikuwa wakiadhirika sana wakati wakienda hospitali kujifungua, wengine hujifungulia njiani na wengine kupoteza maisha, huku wanafunzi wakishindwa kwenda shule.
Mkazi wa kijiji cha Mchangani-Misegese, wilayani Malinyi Mbugani (49), ameishukuru serikali kwa ujenzi huo, sababu limekuwa mkombozi kwao kwa kuwaepusha kupanda kwenye mitumbwi na kutishia uhai wao huku wajawazito wasiozidi 10 wakipoteza kwa kushindwa kuvuka mto huo Maisha hasa wakati wa Mvua za Masika.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo Meneja wa Wakala ya Barabara za Vijiji na Mijini (TARURA) Mhandisi Charles Mangela, anasema barabara hiyo na karavati yamejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 199.9
Anasema mradi huo ulitokana na uharibifu uliotokea kutokana na mvua za masika elnino na kimbunga hidaya zilizonyesha kati ya mwezi Novemva 2023 hadi Mei 2024 na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara katika wilaya ikiwamo na sehemu ya barabara hiyo ya Lugala Misegese.
Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi, amesema ujenzi wa karavati la mawe kwenye daraja hilo unaonesha upendo na kujali kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye naye anapaswa kuoneshwa upendo na wananchi kwa kusimamia na kulinda miradi ya maendeleo iliyopo iwafikie vizazi hata vizazi.
Akiwa kwenye Halmashauri ya Mlimba wilayani Kilombero Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa, Ussi, amezindua daraja la chuma Luipa na ujenzi wa barabara ya Kisegese -Chiwachiwa-Lavena lililojengwa kwa kiwango cha changarawe na udongo kwa kilometa 5.6 iliyogharimu shilingi bilioni 1.926.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED