Bunge limeelezwa kuwa katika mwaka wa fedha 2023/24, jumla ya watumishi 9,384 wa kada ya afya waliajiriwa na kupangiwa kazi katika vituo vya kutolea huduma za afya katika Halmashauri zote nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk. Festo Dugange, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mariam Kisangi.
Katika swali lake la msingi, Mbunge huyo alitaka kufahamu mpango wa serikali wa kupeleka watumishi katika Kituo cha Afya Kilakala kilichopo Manispaa ya Temeke.
Akijibu swali hilo, Dk. Dugange amesema kuwa serikali imeendelea kuajiri watumishi wa kada ya afya na kuwapeleka katika vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki za afya.
“Katika mwaka wa fedha 2023/24, jumla ya watumishi 9,384 waliajiriwa na kupangiwa kazi katika vituo vya kutolea huduma katika Halmashauri, ambapo watumishi wa afya 69 walipangwa katika Manispaa ya Temeke na watumishi watatu katika Kituo cha Afya Kilakala,” amesema Dk. Dugange.
Ameongeza kuwa sambamba na ajira kutoka Serikali Kuu, Manispaa ya Temeke nayo imeajiri kwa mkataba watumishi watatu na kuwapangia majukumu katika Kituo cha Afya Kilakala, ambacho kwa sasa kina jumla ya watumishi 19 kati ya 35 wanaohitajika.
Aidha, Dk. Dugange amesema serikali itaendelea kutoa vibali vya ajira kwa kada za afya na kuwapanga katika Halmashauri zenye upungufu wa watumishi kote nchini ili kuhakikisha huduma bora za afya zinawafikia wananchi wote.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED