Serikali imepanga kutumia Shilingi bilioni 29.1 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mbalimbali za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) katika mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa awamu ya pili ya Mradi wa Vitambulisho vya Taifa.
Ujenzi huo utahusisha ofisi za usajili katika wilaya 31, jengo la makao makuu ya NIDA jijini Dodoma, pamoja na kituo cha matengenezo ya vifaa vya TEHAMA.
Hayo yameelezwa leo bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo, wakati akijibu swali la Mbunge wa Wingwi (CCM), Omari Kombo, ambaye alitaka kufahamu ni lini serikali itajenga ofisi ya NIDA katika Wilaya ya Micheweni.
Akijibu swali hilo, Sillo amesema kuwa NIDA inaendelea kutekeleza awamu ya pili ya Mradi wa Vitambulisho vya Taifa, ambao pamoja na mambo mengine unahusisha ujenzi wa miundombinu muhimu kwa ajili ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
“Kwa sasa utekelezaji wa mradi huu upo katika hatua ya usanifu wa michoro ya majengo na miundombinu ya TEHAMA, sambamba na maandalizi ya kumpata mkandarasi,” amesema Sillo.
Ameongeza kuwa ujenzi wa majengo hayo unatarajiwa kufanyika kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo kiasi cha Shilingi bilioni 29.1 kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa ofisi ya NIDA katika Wilaya ya Micheweni.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED