Zaidi ya watu 50 wamefariki dunia na mamia hawajulikani walipo baada ya boti iliyokuwa imebeba abiria zaidi ya 450 kuzama kufuatia moto uliotokea Jumanne usiku katika Mto Congo, karibu na mji wa Mbandaka, Kaskazini Magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kwa mujibu wa Kamishna wa Usimamizi wa Mto Congo, Competent Loyoko, moto ulisababishwa na abiria aliyewasha jiko la mkaa ndani ya boti hiyo ya mbao. Abiria wengi, hususan wanawake na watoto, walijaribu kujiokoa kwa kuruka majini lakini walikosa ujuzi wa kuogelea.
Timu za uokoaji zikishirikiana na Msalaba Mwekundu zimeendelea na juhudi za kuwaokoa manusura, ambapo takriban watu 100 wameokolewa na kupelekwa kwenye makazi ya dharura mjini Mbandaka.
Ajali za mara kwa mara za vyombo vya majini nchini DRC zimekuwa zikihusishwa na ukosefu wa vifaa vya dharura na matumizi ya vyombo visivyo salama. Mwandishi wa Al Jazeera, Alain Uaykani, amesema bado kuna changamoto kubwa katika usalama wa usafiri wa majini nchini humo.
Desemba 2024, watu 38 walipoteza maisha kwenye ajali ya kivuko, na mwezi Oktoba, watu 78 walikufa baada ya boti kuzama Ziwa Kivu, Mashariki mwa DRC.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED